8 C
New York

Tumieni ubunifu kusaidia utatuzi wa Migongano ya Binadamu na Wanyamapori

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini-Bagamoyo

Waandishi wa Habari nchini hususan wanaoandika habari zinazohusu mazingira wametakiwa kuongeza ubunifu ikiwamo kutumia nyenzo za kisasa ili kuweza kusaidia kutatua migongano ya Binadamu na Wanyamapori ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara.

Ushauri huo umetolewa leo Februari 22 mjini Bagamoyo mkoani Pwani na Mkufunzi Mshauri wa Masuala ya Habari nchini, Pili Mtambalike wakati wa warsha ya kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari kuhusu Migongano ya Binadamu na Wanyamapori Tanzania iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa ufadhili wa  Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani (BMZ) huku mtekelezaji akiwa ni Wizara ya Maliasili na Utalii nchini(MNRT).

Mafunzo hayo ni sehemu ya Mradi wa mwaka mmoja wa Kupunguza Migongano ya Binadamu na Wanyamapori Tanzania utakaotekelezwa katika Ukanda wa Ruvuma.

Mtambalike amesema iwapo waandishi wa habari watatumia ubunifu katika kuandika changamoto zinazotokana na migongano ya Binadamu na Wanyamapori kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuwaamsha wafanya maamuzi kuja na majibu kwa haraka.

“Tumieni ubunifu wenu katika kuandika habari ili muweze kusaidia watunga sera kufanya maamuzi kwa haraka hasa katika changamoto hizi za migongano ya binadamu na wanyamapori, mna nafasi ya kuhoji kupitia makala zenu mnazoandika.

“Hivyo, kama waandishi wa habari mnawajibu wa kuamua kutunza mazingira huku mkizingatia kusoma sana juu ya migongano ya binadamu na wanyamapori kwa ajili ya kusaidia jamii yetu kupata uelewa na kukuza sekta ya uhifadhi nchini kwani waandishi wa habari ni nguzo muhimu katika kutatua changamoto.

“Kuna nyanja pia ya kutumia eneo la uandishi wa habari za takwimu (DATA) ambapo eneo hili iwapo litatumika vizuri litasaidi kushawishi watunga sera ambao ni Serikali kutoa majibu ya changamoto mbalimbali,” amesema Mtambalike.

Mwenyekiti wa JET, Dk. Ellen Otaru.

Akizungumzia kuhusu Mradi huo wa Kupunguza Migongano ya Binadamu na Wanyamapori Tanzania utakaotekelezwa katika Ukanda wa Ruvuma, Mwenyekiti wa JET, Dk. Ellen Otaru amesema mradi huo wa mwaka mmoja umeanza kutekelezwa Desemba 2023 ikiwa ni mahususi kwa ajili ya kuangalia migongano iliyopo kati ya binadamu na wanyamapori.

“JET kwa kushirikiana na wadau inawezesha waandishi wa habari kupata mafunzo ili baadae waweze kutengeneza habari na makala zitakazosaidia kupunguza madhara yatokanayo na migongano ya binadamu na wanyamapori.

“Hii itakuwa ni pamoja na kutoa uelewa kwa wananchi kupitia taaluma zetu kuhusu masuala ya migongano hii ya binadamu na wanyama pori ikiwa na maana ya kuandika kwa umakini, baada ya kupata taarifa kwa kina kutoka kwa watu sahihi ikiwamo data,” amesema Dk. Ellen.

Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo alizitaja wilaya zilizolengwa katika mradi huo kuwa ni Mkoa wa Lindi na Ruvuma.

“Mradi utatekelezwa na wadau mbalimbali. Walengwa ni wakazi wa vijijini vilivyoko kusini mwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na Pori la Akiba la Selous, katika wilaya za Liwale (Mkoa wa Lindi), Namtumbo na Tunduru (Mkoa wa Ruvuma),” amesema Chikomo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img