Na Mwandishi Wetu, Gazetini
KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imewaaga na kuwapatia vyeti wanafunzi 50 kutoka vyuo vikuu waliokuwa wanafanya kazi katika mgodi huo kupitia Mpango wa Mafunzo Kazini kwa mwaka 2023.
Wanafunzi hao ambao 30 ni wa kike na 20 wa kiume, waliopokewa Februari mwaka jana, wameagwa mwishoni mwa iliyopita mkoani Geita.
Hata hivyo, kati yao 15 wamefanikiwa kubaki ndani ya kampuni hiyo ambapo watano wamepatiwa mkataba wa kudumu huku 10 wakipatiwa mkataba wa muda chini ya taratibu za program hiyo ya wahitimu.
Hatua hiyo ni mwendelezo wa mpango wa GGML wa kuchukua wanafunzi wa vyuo vikuu na kuwapatia uzoefu wa kufanya kazi katika fani mbalimbali ndani ya mgodi huo kwa lengo la kuunga mkono mipango ya serikali ya kuimarisha uwezo wa wahitimu kuajiriwa.
Akizungumza katika hafla ya kuwaaga wahitimu hao, mwishoni mwa wiki mkoani Geita, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong amewapongeza wanafunzi hao kwa kudumisha uweledi na juhudi katika kazi walizokuwa wakizifanya kwa kipindi cha mwaka mmoja ndani ya mgodi huo.
Amesema wanafunzi hao walikuwa wakijituma kwa bidii na kuonesha uwezo wao katika nyanja mbalimbali walizokuwa wamepangiwa na wasimamizi wao ndani ya GGML.
Aidha, amewaomba waende kuwa mabalozi wema katika kuitangaza GGML kwa yale mema yote waliyojifunza kipindi chote cha mwaka mzima.
Sambamba na hayo Terry amesema GGML itachukua wanafunzi 40 katika mpango huo wa kuwapatia mafunzo kwa mwaka huu wa 2024. Kati yao 20 watakuwa wa kike na 20 wa kiume.
Wakizungumza baada ya kumaliza mafunzo hayo, mmoja wa wanafunzi hao, Julieth Lwehabura ameishukuru GGML kwa kuwapokea na kuwapatia uzoefu wa kipekee ambao utakuwa chachu kwao katika kuendelea kupiga hatua katika taaluma zao.
Naye Shamimu Mfinanga alisema uzoefu walioupata ndani ya GGML unakwenda kufungua milango ya fursa kwao hasa ikizingatiwa hiyo ni kampuni kubwa ambayo imejitolea kuwa mfano wa kuigwa kwa kuwajali wanafunzi wanaohitimu vyuo vikuu nchini.
Tangu kuanza kwa program hiyo mwaka 2009, GGML imeshatoa mafunzo kwa wanafunzi 218 kutoka vyuo mbalimbali kati yao wanawake 131 na wanaume 87.