20.4 C
New York

Shoroba za Derema-Amani Nilo zitakavyochochea ustawi wa wanyama Tanzania

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini

Serikali iko katika mbioni kuunganisha Shoroba mbili za Derema na Amani Nilo zinazopatikana ndani ya hifadhi ya Taifa ya Mazingira Asilia ya Amani iliyoko Wilaya za Muheza na Korogwe mkoani Tanga.

Hatua hiyo siyo tu itasaidia kuongezeka kwa wanyama lakini pia itakuwa mwarobaini wa kudhibiti migogoro kati ya binadamu na wanyama.

Alphonce Nyululu ni Kaimu Mhifadhi katika Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Amani Nilo.

Alphonce Nyululu ni Kaimu Mhifadhi katika Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Amani Nilo, ambapo akizungumzia mpango wa Serikali wa kuzinunganisha shoroba hizo anaseman kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuchochea wanayama waweze kuzaliana kwa wingi.

“Sasahivi kuna mpango wa kuunganisha hifadhi hii ya mazingira kupitia Derema mpaka Amani Nilo ili wanyama waweze kuzaliana na wakiwa na nafasi salama.

“Kwa hiyo kuna utaratibu wa kuhakikisha kwamba wananchi hawa wanaoishi katika maenoe hayo ndani ya ushoroba wa Derema wanakaa pembeni ili kuruhusu mimea iweze kuota na kupanda miti mbalibali, pia itatoa fursa nzuri kwa  wanyama waweze kutoka sehemu mmoja kwenda nyingine,” anasema Nyululu.

Kulingana na mtaalamu huyo, kuunganishwa kwa shoroba hizo kutachochea kwanza, wanyama na viumbe mbalimbali kuweza kuzaliana kwa wingi kwani uwepo wa makazi ya binadamu ndani ya shoroba ni kikwazo.

Akizungumzia urefu wa mpaka wa shoroba ya Amani anasema kuwa ni kilometa 149.

Chanzo cha maarifa kwa wanafunzi

Jumanne Nyange ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Antakae ambaye anasema kuwa ushoroba walionao ni ule wa Derema unaounganisha msitu wa Amani na ule wa Nilo ambao unazungukwa na kata za Kisiwani na Kwezitu.

“Huu ushoroba ni njia ambayo inapitiwa na wanayama pamoja na ndege, hapa shuleni kwetu tayari tuna ramani ambayo tunaitumia kuwafundisha wanafunzi kuelewa mipaka iliyopakana na shoroba hii.

“Hivyo, imekuwa ni msaada kwetu kuwasaidia wanafunzi kujua kwamba shule yao au kijiji chao kimepakana na nani, hii ni elimu ambayo tumeanza kuitoa Machi, 2023 na imekuwa na mafanikio makubwa na wanafunzi wengi wamekuwa na mwitikio mzuri wa somo hili,” anasema Nyange.

Wanafunzi wanasemaje?

Idrisa Said ni Mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya Msingi Antakae ambaye anasema kwasasa anao uwezo wa kuuelezea vizuri ushoroba wa Amani Nilo kutokana na kupata maarifa kutoka kwa walimu wake.

“Kwasasa tunafahamu kwamba sehemu gani ni mapitio ya wanyama na hivyo kuna baadhi ya mambo ambayo kama wanajamii hatutakiwi kufanya ikiwamo kukata miti ndani ya shoroba.

“Hivyo, ndiyo sababu hata mimi kwa maarifa niliyoyapata nikikuta mtu anaharibu mazingira kwanza nitamuelimisha juu ya kile anachokifanya kisha akikaidi nitamripoti katika mamlaka husika ili aweze kuchukuliwa hatua zaidi nakuwa fundisho kwa watu wengine,” anasema.

Upande wake, Haji Joseph anasema kuna umuhimu kwa wanafunzi kuanza kufundishwa kuhusu ushoroba mapema kwani unawasaidia kuwa mabalozi wazuri wa mazingira.

“Kupata elimu mapema kuhusu shoroba kunasaidia kutokuwinda wanyama, ndege ovyo pia kutunza mazingira yetu kwa ajili ya kuendelea kuvutia viumbe hai kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha baadae,” anasema Joseph.

Mwenyekiti Magoda

Issa Msikiti ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Magoda Msasa kilichopo Kata ya Kisiwani Tarafa ya Amani ambaye anasema wao ndiyo wadau wakuu waliojitoa kupisha ardhi yao kwa ajili ya kuwapatia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa ajili ya shoroba.

“Sisi ndiyo tumekuwa wadau wakuu wa kuhakikisha kwamba msitu wetu unakuwa imara na shoroba zetu za Derema na Amani Nilo zinakuwa salama kwa ajili ya ustawi wa wanyama.

“Hii imeongeza kuwa kivutio kwa wanyama na ndege kuongezeka hatua ambayo inaendelea kuchochea utalii, hivyo sisi wananchi tumekuwa walinzi wa shoroba zetu hizi kuhakikisha kwamba haziharibiwi wala kuvamiwa,” anasema Msikiti.

Anasema kuwa kwa watu ambao wamekuwa wakivuka mipaka na kuingia ndani ya shoroba hizo wamekuwa wakichukuliwa hatua kali.

“Kwanza kabisa mwananchi hatakiwi kuingia kabisa ndani ya eneo la shoroba na atakayebainika anaweza hata kuhama bila kutaka, ndiyo maana kwa mwezi hapa tunafanya doria mara moja mpaka mara tatu pindi kunapokuwa na hali ya watu kuvamia,” anasema.

JET

John Chikomo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) ambapo akizungumzia shoroba ya Amani Nilo anasema kuwa ni muhimu sana katika uhifadhi wa bayonuai nchini.

“Tumekuja kwenye msitu wa Amani kwa ajili ya kuangalia shoroba ya Amani Nilo kwani tunajua kwamba kuna kamati ambayo imeanzishwa kwa ajili ya kuongoa shoroba mbalimbali nchini.

“Kwani kama tunavyojua kwamba Amani Nilo ni moja ya shoroba ambazo ni muhimu sana kwa uhifadhi wa bayoanuai hapa nchini.

“Tunaelewa kwamba nchi yetu imesaini mikataba ya kimataifa na ule wa bayoanuai  ukiwa ni mmoja wapo na eneo hili ni maarufu na bora sana katika masuala ya uhifadhi wa bayoanuai, kwa hiyo tunaamini kwamba kwa kuongoa shoroba hii ya Amani Nilo masuala ambayo nchi inapigia kelele yatafanyika kwa umakini zaidi,” anasema Chikomo na kuongeza kuwa:

“Pia, tumeona kwamba shoroba hii ya Amani Nilo inavutia watalii kwani ina vivutio mbalimbali ambavyo havipatikani sehemu nyingine, mfano tumeona vinyonga ambao wanapatikana katika shoroba hii, bundi wa pekee na aina mbalimbali za ndege ambao katika dawati la IUCN wamewaainishwa kuwa wako hatarini kutoweka na wanapatikana katika eneo hili.

“Kwa hiyo kuna umuhimu mkubwa kwa timu ya waandishi wa habari kuelezea umma wa Watanzania juu ya vivutio vilivyopo katika shoroba hii lakini pia kazi kubwa ambayo inafanyika na wadau mbalimbali kuhakikisha shoroba hii inabaki katika uhalisia wake,” anasema Chikomo.

Aidha, Chikomo anakiri kuwa JET inaridhika na juhudi kubwa ambazo zinafanyika ikiwamo wadau mbalimbali ikiwamo Serikali.

“Serikali imeweka mkono wake mkubwa sana kuhakikisha inaongoa shoroba kwani utaona kwamba kuna kamati ya kitaifa ya kuongoa shoroba imeanzishwa kwa hiyo hiyo ni kilelezo kuonyesha kwamba juhudi mbalimbali zinfanyika.

“Lakini ukiacha hilo kuna wafadhili kama USAID kupitia mradi wa Tuhifadhi Maliasili kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kazi ainzofanywa na wadau kwa ajili ya kuongoa shoroba zinafanyika, hivyo JET tunaamini kwamba juhudi hizi zikifanywa kwa pamoja na wadau mbalimbali na waandishi wa habari wakatumia kalamu zao kutangaza kazi kubwa ambayo inafanyika basi tutafikia malengo tuliyojiwekea,” anasema Chikomo.

Juni, mwaka huu, akielezea hali ya Shoroba nchini, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Fortunata Msoffe alisema shoroba nyingi nchini zinakabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo ongezeko la shughuli za kibinadamu kwenye maeneo hayo.

Alifafanua kuwa kutokana na hali hiyo Serikali imeamua kuanza kutekeleza mpango wa kuongoa shoroba hizo kwa kipindi cha miaka mitano ambapo mpango huo ulizinduliwa na wizara Septemba 17, 2022.

“Tumeanza na shoroba za kipaumbele ambazo zilitokana na kazi iliyofanywa na wadau wa maendeleo wakishirikiana na wizara pamoja na wataalam mbalimbali katika kuainisha shoroba ili kupunguza matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu kwenye makazi ya watu,” alisema Dk. Msoffe.

Aidha, Dk. Msoffe alisema katika mpango huo Serikali imeamua kuanza na zile shoroba 20 ambazo zipo hatarini kutoweka.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img