21 C
New York

Visual| Kila mmoja anawajibika kuepusha athari za wanyamapori

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini

Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti Migogoro ya Binadamu – Wanyamapori 2020 – 2024, Watanzania 560 waliuawa na simba katika kipindi cha mwaka 1990 hadi 2004 huku wengine 308 wakijeruhiwa.

Hii ni sawa na kusema kwamba kila mwaka takribani watanzania 40 walikuwa wakipoteza maisha kwa kushambuliwa na simba wastani wa watu watatu kila mwezi. Kiwango hicho ni cha juu zaidi ikilinganishwa na athari zinazotokana na wanyama wengine.

Takwimu hizo zinaendelea kuchambua kwamba kati ya mwaka 2012 hadi 2019 Watanzania 1,069 wamefariki dunia kwa kushambuliwa na wanyama. Aidha, katika kipindi hichohicho Watanzania 204 wamepata ulemavu wa kudumu huku mifugo 792 ikifa.

MwakaVifo vya BinadamuUlemavu wa kudumuMajeruhiWanyama waliokufaHeka za mazao zilizoharibiwa
2012/13692338461,518
2013/14613149934,046
2014/155920411076,786
2015/161022078648,924
2016/1713230541304,567
2017/1838020291495,016
2018/192666014920310,547
Jumla1,06920443879241,404
Matukio ya migogoro kati ya binadamu na wanyama yaliyoripotiwa kutoka 2012 hadi 2019

Mbali na madhara hayo ya binadamu na wanyama kupoteza maisha na kujeruhiwa, hekari za mazao 41,404 ziliharibiwa na wanyamapori kati ya mwaka 2012 hadi 2019.

Hatua hizo zote zimesababisha hasara kwa Serikali kwani ililazimika kutumia Sh bilioni 4.67 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wahanga wa wanyama hao.

Licha ya kwamba ushirikiano kati ya binadamu na wanyamapori ni kipaumbele cha kitaifa kwa maendeleo endelevu na uhifadhi wa wanyamapori nchini Tanzania.

Lakini ongezeko la idadi ya watu linalohusiana na mahitaji ya ardhi na maliasili ni changamoto kubwa kwa sasa inayotishia ustawi wa wanayama hao.

Takwimu zinaonyesha kwamba idadi ya watu nchini Tanzania inaongezeka kwa kasi ya zaidi ya 4% kwa mwaka.
Kwani inakadiriwa kwamba idadi ya watu nchini Tanzania itafikia 89,204,781 ifikapo mwaka 2035.

Idadi hiyo ya watu inatajwa kuongezeka ilihali kwamba ardhi ikisalia kuwa ileile hatua inayoibua mgogoro kati ya binadamu na wanyamapori.

Tunashuhudia katika miaka ya karibuni wanyama kama tembo wakisababisha athari katika maeneo mbalimbali nchini hatua inayotokana na kuzibwa kwa mapito ya wanyama hao(shoroba).

John Noronha ni Meneja Ufuatiliaji na Tathmini kutoka mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili ambapo akizungumza hivi karibuni katika warsha ya kuwajengea uwezo wanahabari juu ya umuhimu wa shoroba iliyofanyika mjini Bagamoyo kwa uratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira(JET) chini ya ufadhili wa USAID kupitia mradi wa Tuhifadhi Maliasili anakiri kuwa kadri watu wanavyozidi kuongezeka ndivyo na ustawi wa wanyamapori unavyoingia shakani na hivyo kuchochea athari mbalimbali.

“Takwimu zinatuonyesha kwamba Watanzania tutakuwa 89,204,781 ifikapo mwaka 2035, changamoto inakuja kwamba kuongezeka kwa idadi hiyo tutahitaji ardhi kwa ajili ya kilimo, ardhi kwa ajili ya makazi, raslimali kwa ajili ya nishati.

“Kwa hiyo hivi vyote vinasababisha muingiliano baina ya binadamu na wanyamapori, kwani hata wanyama wenyewe kuna muda wanahitaji usalama, maji, chakula na vitu vingine, hivyo unakuta kwamba kule watakakohitaji kwenda kupata vitu hivyo ndiko binadamu waliko,” anasema Noronha na kuongeza kuwa:

“Changamoto nyingine ni uhaba wa maji ambalo hili limekuwa ni tatizo kubwa siyo kwa binadamu tu bali hata kwa wanyama wenyewe kwani maji hakuna hivyo wanalazimika wanyama kama mamba, vikobo na wengine wanaingia kwenye maeneo waliko binadamu hivyo kusababisha maafa, hivyo kuchepusha maji ya kwenye mito ni moja ya sabahu kubwa inayoleta madhara kwa binadamu,” anasema mtaalamu huyo kutoka USAID.

Shughuli za kilimo zinavyozidi kushamiri ndani ya maeneo ya hifadhi.

Anataja eneo jingine linalosababisha migongano baina ya wanyamapori na binadamu kuwa ni kupuuzwa kwa sheria kwani licha ya sheria kukataza kulimwa kwa baadhi ya maeneo lakini baadhi ya wakulima kutokana na uhaba wa ardhi wamekuwa wakikiuka maelekeoz hayo na hivyo kuleta madhara.

“Jingine ni hili la mabadiliko ya tabianchi ambapo hii imekuwa ikisababisha wanyama kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine hatua ambayo imekuwa na madhara makubwa,” anasema Noronha.

Ni wajibu wa kila mtu kuepusha athari

Dk. Ellen Otaru ni Mwenyekiti wa JET ambapo anasema kuwa ni wajibu wa kila mmoja kusaidia kuepusha athari zinazotikana na muingiliano wa binadamu na wanyama nchini hususan katika maeneo ambayo ni mapitio ya wanyama(shoroba).

“Nijukumu la kila mmoja wetu wakiwamo waandishi wa habari kuhakikisha kuwa tunakuwa kuwa mstari wa mbele kuibua na kuelimisha jamii juu ya athari zitokanazo na shughuli za kibinadamu kama kilimo na nyinginezo ndani ya shoroba pamoja na faida za kiuchumi zinazopatikana.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), Dk. Ellen Otaru akifafanua jambo wakati wa mafunzo hayo.

“Kwani ukiangalia kwa miaka ya karibuni kumekuwa na athari zinazosababishwa na wanayama ambazo kwa kiasi kikubwa zinaweza kuzuilika iwapo jamii itakuwa na uelewa wa kutosha,” anasema Dk. Otaru.

Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo anasema kwamba jamii inahitaji uelewa juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira hususan mapitio ya wanyama(shoroba).

“Lengo la JET ni kuona vyombo vya habari nchini vinabeba ajenda hii ya uhifadhi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuonyesha athari zilizopo iwapo shoroba hizi hazitatunzwa, lakini pia kuonyesha faida zilizpo ndani ya shoroba hizi.

“Tunaona kuwa sababu ya maendeleo mapitio mengi ya wanyama yamefungwa kutokana na ujenzi, hivyo ndiyo sababu tunataka mapitio ya wanyama yawe wazi,” anasema Chikomo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img