8.5 C
New York

Makala| Ukosefu wa mikakati unavyoinyima Tanzania utajiri kupitia shoroba

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini

Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Sekta ya Utalii nchini inachangia asilimia 17.5 ya Pato la Taifa.
Kama hiyo haitoshi sekta hiyo inachangia asilimia 25 ya fedha za kigeni huku ikitoa ajira za moja kwa mojua 600,000 na nyingine 2,000,000.

Hata hivyo, pamoja na manufaa hayo yanayopatikana bado kuna sehemu kubwa ya fedha ambayo taifa linapoteza kutokana na kukosekana kwa mikakati thabiti ya udhibiti wa Shoroba.

Lakini je Shoroba ni nini?

Dk. Elikana Kalumanga Ngallaba ni Meneja Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, ambaye anatafsiri kuwa Shoroba ni maeneo ambayo yanaunganisha hifadhi za wanyamapori au misitu.

Akizungumza katika Warsha ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Wanahabari kuhusu Mradi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) wa Tuhifadhi Maliasili uliofanyika mjini Bagamoyo mkoani Pwani, Dk. Kalumanga anasema kuwa kwa tafsiri nyingine, shoroba ni maeneo yanayounganisha maeneo yaliyohifadhiwa ambayo mara nyingi yanapitiwa na wanyamapori na shughuli nyingine ambazo wananchi wanafanya ikiwamo huduma za maji na kiuchumi.

Nini faida ya Shoroba

Dk. Kalumanga anasema kuwa faida za shoroba zimegawanyika katika makundi makubwa matatu ambayo ni kiikolojia, kiuchumi na kijamii.

“Katika eneo la ikolojia na kimazingira shoroba zinasaidia wanyamapori au viumbe kupita kutoka eneo moja kwenda jingine pindi wanapokuwa wanatafuta mahitaji yao kama maji, marisho na hifadhi kwa ujumla.

“Tukiangalia kijamii kuna faida nyingi ambazo wananchi wanapata kupitia shoroba hizi ikiwemo kuni, dawa na huduma nyingine.
“Mfano ukiangalia shoroba inayoitwa Raja inayotoka hifadhi ya taifa ya Manyara kuelekea hifadhi ya Ngorongoro utakuta kuna ndugu zetu Wahadzabe na jamii nyingine ambao wanaishi huko na wanazitegemea kwa ajili ya chakula, kipato na makazi.

“Tukiangalia kiuchumi sababu kuna uwepo wa wanayamapori na uzuri wa baadhi ya maeneo haya yanavutia watalii, kwahiyo kuna faida ya kiuchumi inayotokana na utalii unaofanyika kwenye maeneo haya kwa mfano ukichukulia shoroba ya Kwakuchinja ambayo inaunganisha hifadhi ya taifa ya Tarangire na ile ya Ziwa Manyara ambapo ndani kuna eneo la uhifadhi wa jamii la Burunge ambapo kuna uwekezaji kubwa ikiwamo hoteli ambazo zimeajiri wafanyakazi, maduka na huduma nyingine ambazo zinatumiwa na watalii na hivyo kuongeza kipato kwa wananchi na taifa kwa ujumla kwa hiyo hizo ni moja ya faida kubwa zinazopatikana kupitia shoroba,” anasema Dk. Kalumanga.

Hali ya shoroba nchini

Akizungumzia hali ya shoroba nchini anasema kuwa kuna changamoto zake ikiwamo ya udhibiti hafifu.

Anasema zipo baadhi ambazo zinapatika na zile ambazo takwimu za Serikali zinaonyesha kuwa zimetoweka kutokana na shughuli za wananchi zisizo endelevu.

“Kwa kifupi tunaweza kusema hali ya shoroba nchini siyo nzuri sana,” anasema.

Hata hivyo, Dk. Kalumanga anaitaja changamoto ya kukosekana kwa mikakati kuhusu uhifadhi wa shoroba nchini kuwa ni moja ya sababu iliyosababisha baadhi ya wananchi kuvamia maeneo hayo muhimu na kuanzisha shughuli za kilimo ikiwamo makazi.

“Hii inasababishwa na shoroba nyingi kutojulikana kutokana na kutokuainishwa kabla kwa wananchi, hivyo watu wamekwenda wakaweka makazi wakaanzisha na shughuli za kilimo sababu zilikuwa hazitambuliki.

“Pili zipo shoroba zilizokuwa zinatambulika na wanyama wanapita katika maeneo hayo, lakini hapakuwa na mikakati au mipango ambayo ilikuwa inaelekeza namna gani haya maeneo yahifadhiwe nafikiri ndiyo sababu serikali inakuja na mikakati ya namna gani shoroba hizi zinatakiwa zihifadhiwe ili kuwe na maendeleo endelevu sababu ya umuhimu wake kiuchumi, kijamii na katika nyanja ya mazingira na kiikolojia,” anasema Dk. Kalumanga.

Kwa mujibu wake, iwapo shoroba zitatoweka uwezekano wa kuzirejesha upo.

“Hata kama imeharibika uwezekano wa kuirejesha upo na ndiyo sababu kuna juhudi kubwa za kurejesha shoroba hizi katika uhalisia wake.

“Pia taasisi mbalimbali kwa kushirikiana na serikali zinaweka nguvu katika kurejesha shoroba hizi na moja ni shoroba inayounganisha hifadhi ya taifa ya Udzungwa,Mwalimu Nyerere na pori la akiba la Selous kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili,” amesema Kalumanga.

John Noronha ni Meneja Ufuatiliaji na Tathmini kutoka mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili ambapo anasema kuwa kutokana na changamoto hizo USAID ilikuja na mradi wa miaka mitano wa kuangalia changmoto zinazo wakabili wanyama katika shoroba(mapitio ya wanyama) hapa nchini.

“Hivyo, mradi huu unajikita kuangalia mapitio ya wanyama nchini na changamoto zilizopo pale na tunajitahidi kuzitatua kwa ajili ya uhifadhi endelevu wa maliasili hususan wanyama pori.

“Hilo ndilo lengo kuu la mradi huu wa miaka mitano na ulianza Juni, 2021 hadi sasa una miaka miwili na miezi sita,” anasema Noronha.

Akizungumzia malengo ya mradi huo wenye thamani ya dola milioni 30, Noronha anasema kuwa lengo la kwanza ni kujenga uwezo kwa taasisi za umma na binafsi zikiwamo idara za wanyamapori na vyuo.

“Moja ya uwezo ni kuhakikisha kuwa tukiwapa fedha tunawahimiza kwenda kusoma kwa ajili ya kuongeza uelewa huku pia tukitoa msaada wa vifaa muhimu kama kompyuta na vingine.

“Lengo la pili ni ushiriki wa sekta binafasi ambapo lengo moja la mradi huu ni kuhakikisha kuwa taasisi binafsi zinashirikishwa kwani zimekuwa zikiachwa nyuma licha ya ukweli kwamba nazo zinachangia katika sekta hii ya uhifadhi kwani ndiyo wawekezaji wakubwa.

“Lengo la tatu ni kuboresha sera kwani tunajua nchi yetu inaongoza na sera lakini katika sekta yetu kuna wadau wengi hivyo tunaangalia sera zilizopo kama zinaendana na kwa maeneo ambayo hayana sera kabisa tunajitahidi kuhakikisha yana sera, katika malengo haya yote tumekuwa tukijitahidi kushirikisha wadau wote na miongoni mwao ni Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira(JET) ambao tumekuwa tukishirikiana kwa ukaribu,” anasema Noronha na kusisitiza kuwa JET imekuwa na msaada mkubwa katika kutekeleza mradi huo.

John Noronha Meneja Ufuatiliaji na Tathmini kutoka mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili akizungumza hivi karibuni katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wanahabari juu ya shoroba.

Shoroba zinazolengwa

Noronha anasema pamoja na Tanzania kuwa na shoroba zaidi ya 60 lakini mradi huo umejikita katika shoroba saba kwa sasa ambazo ni Kwakuchinja inayounganisha Tarangire na Manyara.

“Pia, tuna shoroba ya Amani Hill iliyoko Muheza, Tanga nyingine tunayoipa kipaumbele ni Nyerere, Selous na Udzungwa ambayo inaunganisha hifadhi ya Nyerere na ile ya Udzungwa.

“Nyingine ni Ruaha,Rungwa-Inyonga ambayo ipo katika Wilaya ya Itigi na Sikonge inaunganisha pori la akiba la Rungwa na Inyonga na shoroba nyingine ambayo iko jirani na maeneo hayo ni Ruaha, Rungwa-Katavi,” anasema Noronha.

Anasema kuna shoroba nyingine mbili ambazo moja iko katika wilaya ya Tanganyika na Uvinza inayofahamika kama Mahare-Katavi ambayo inaunganisha hifadhi hizo mbili.

“Shoroba ya saba ni Kigosi, Moyowosi-Burigi Chato ambayo iko wilaya ya Biharamlo na Kakonko.Hivyo haya ni maeneo ambayo mradi huu unayalenga kuyafanyia kazi,” anasema Noronha na kuongeza kuwa maeneo hayo yakihifadhiwa vizuri basi yanaweza kuwa na msaada mkubwa kwa nchi ikiwamo kutunza mazingira na kuchochea hewa safi.

John Chikomo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira nchini(JET) ambapo akizungumzia Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili anasema kuwa ni muhimu kutunza shoroba hizo kwani zitachochea kukuza utalii ndani ya nchi yetu.

“Imeonekana kwamba kwa kutunza shoroba hizi kuna manufaa makubwa kuanzia kukuza utalii ndani ya nchi yetu ambao utachochea kuimarisha uchumi wa nchi.

John Chikomo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira nchini(JET) akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wanahabari kuhusu shoroba yaliyofanyika Bagamoyo mkoani Pwani.

“Pamoja na hayo shoroba hizi zinamanufaa makubwa katika kukuza ikolojia na kusaidia jamii, tumeona kwamba kuna baadhi ya shoroba ambazo ndani yake kuna makazi na hata uwekezaji wa hoteli ambao unasaidia kutoa ajira kwa Watanzania.

“Hivyo, kila mmoja wetu kwenye nafasi yake anao wajibu wa kuona umuhimu wa kutunza shoroba zetu,” anasema Chikomo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img