Na Winfrida Mtoi, Gazetini
Kampuni ya magari ya TATA Tanzania imezindua mpango maalum kwa ajili ya sekta ya usafirishaji wa mizigo mikubwa nchini kwa kuzindua Trela za mizigo aina ya ‘Tiva Trela’ ili kumrahisishia mfanyabiashara na mkulima katika kupakia mizigo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi uliofanyika kwenye ofisi za kampuni hiyo Vingunguti jijini Dar es Salaam, Meneja Mauzo na Masoko, Smart Deus amesema lengo la mpango huo ni kuwaweka karibu wateja na kampuni katika msimu huu wa mauzo na mavuno nchini ambapo magari hayo yanapatikana kwa mkopo pia.
” Uzinduzi huu umeambatana na uzinduzi wa Trela ya kubebea mizigo mikubwa kwa wakati mmoja. Pia tumeandaa mpango maalumu kwa wateja watakaowahi kipindi hiki cha mwanzo kielekea msimu wa mauzo,” amesema.

Ameeleza kuwa kuanzia mwaka 2021 hadi 2024 katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, umekuwa ni wakati mzuri biashara kutokana na milango ya kibiashara kufunguka.
Deus amesema kutokana na hali hiyo wameahidi kushirikiana na Serikali na wadau wao kwa kuleta bidhaa bora zaidi zinazokidhi mahitaji ya watanzania.
Amesema kwa zaidi ya miaka 20 ya kampuni hiyo nchini, wamebaini uwepo wa changamoto katika usafirishaji kulingana na mazingira na barabara , hivyo kuja na suluhisho la kuleta magari yenye uwezo wa kuendana na mazingira hayo.

Naye Meneja Mauzo wa TATA, Kitengo cha Force Motors, Robert Mwakabibi amesema mpango huo haujaacha nyuma usafirishaji wa abiria baada ya kuleta gari salama kupunguza adha ya usafiri na kuwaongezea kipato wamiliki na madereva wa daladala.
Kwa upande wa magari ya shule amesema wamebaini magari mengi hayakutengenezwa na mfumo mzuri kwa ajili ya wanafunzi hali iliyowapa msukumo wa kufanya mapinduzi katika sekta hiyo.
“Ukiangali gari zetu ni tofauti na nyingine, gari nyingi zinaletwa zikiwa zina muda mrefu lakini za kwetu ni gari mpya kabisa. Gari za shule nyingi zilizopo hazijatengezwa maalum kwa ajili ya wanafunzi , sisi tumekuja na mfumo wa kuhudumia wanafunzi wa aina zote, wa kawaida na wenye mahitaji maaalum.
“Kwa kuzingatia changamoto ya usafiri wa abiria, kampuni imeleta gari bora zinazoweza kupunguza adha ya usafiri pamoja na kuongeza kipato cha wamiliki wa daladala. “Tumeona soko linauhitaji mkubwa kwa usafiri wa wanafunzi, taasisi za serikali na binafsi,” ameeleza Mwakibibi.
Amesema wameweka mfumo mzuri wa mteja kupata gari hizo ambapo kuna kulipa fedha taslimu na mkopo kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kifedha.
Akizungumzia jinsi utaratibu mkopo wa magari hayo unavyotolewa, Meneja Mauzo wa kampuni hiyo, Begumisa Egbert, amesema mkopo usio na riba unatakiwa kulipa asilimia 50 na nyingine iliyobaki inalipwa kwa kipindi cha miezi 12.
Ameeleza kuwa mkopo mwingine ambao utakuwa na riba kidogo, unatakiwa kulipa asilimia 20 ya bei ya gari unayotaka, kisha iliyobaki inalipwa kwa kuanzia miezi sita hadi miaka mitatu.