15.8 C
New York

Migogoro ya viongozi yamchefua Dk. Biteko

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amewataka viongozi kote nchini kuweka maslahi ya wananchi mbele na kuacha migogoro inayotokana na ubinafsi wao.

“Hawa Watanzania hawataki migogoro yetu sisi viongozi na wakati mwingine migogoro tuliyonayo ni migogoro ya maslahi binafsi. Tumeacha kuwahudumia wananchi tunashughulikiana, tunataka huyu akwame, huyu afanikiwe kwa sababu tuna ‘cartel’ (makundi),” amesema Dk. Biteko

Akizungumza Aprili 24, 2025 Mundarara, Wilayani Longido, Dk. Biteko amesema kuwa amani ndiyo msingi wa utoaji huduma bora.

 “Tunataka watu waungane, wafanye kazi ya pamoja. Hakuna kitu kinachotia aibu kama unakuta kiongozi umepewa nafasi mahali fulani ama wewe una cheo mahali fulani badala ya kuzungumza shida za watu unawazungumza watu, Huyu kwako mbaya, yule mbaya, huyu mbaya, Wewe ukiulizwa uzuri wako huna cha kuonesha,” amesema.

Amesisitiza kuwa viongozi waliopata nafasi wanapaswa kumtumia mwananchi kama mteja wao wa kwanza, wa pili, na wa tatu.

“Viongozi tuliopata nafasi mteja wetu wa kwanza awe mwananchi, mteja wetu wa pili awe mwananchi, mteja wetu wa tatu awe mwananchi. Hawa wananchi ndiyo wanatupa uhalali wa sisi kuitwa viongozi, tukumbuke ni kwa kodi zao tupo hapa, tusihubiri chuki. ”amesisitiza Dk. Biteko.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img