13.3 C
New York

WHI yaridhishwa na maendeleo ya mradi wa nyumba 101 Mikocheni

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Bodi ya Uwekezaji na Fedha ya Watumishi Housing Investment (WHI) imefanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba 101 unaotekelezwa katika eneo la Mikocheni, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha watumishi wa umma wanapata makazi bora, salama na ya gharama nafuu.

Ziara hiyo iliyofanyika leo Aprili 17, 2025, ilihusisha wajumbe wa bodi ambao walionesha kuridhishwa na kasi ya ujenzi pamoja na viwango vya ubora vinavyotumika katika mradi huo unaogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 18 hadi kukamilika kwake.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Celestine Muganga, alisema kuwa mradi huo ni kielelezo cha utekelezaji wa dira ya WHI katika kusaidia watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla kupata makazi bora.

“Tunatambua kuwa mahitaji ya makazi ni makubwa nchini, hasa kwa watumishi wa kipato cha kati na cha chini. Mradi huu tayari umeshapata wanunuzi na nyumba zote zimeshalipiwa, jambo linalodhihirisha uhitaji mkubwa wa miradi ya aina hii,” alisema Muganga.

Aidha, aliongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo unakwenda sambamba na vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka msukumo mkubwa katika sekta ya makazi kwa wananchi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa WHI, Sephania Solomon, alisema kuwa ujenzi wa nyumba hizo unatarajiwa kukamilika ifikapo Machi 26, 2026. Alisema nyumba hizo zimetengenezwa kwa kuzingatia mahitaji ya wanunuzi, viwango vya ubora wa hali ya juu na mazingira rafiki kwa makazi.

“Nyumba hizi ni za vyumba kimoja, viwili na vitatu, na zimebuniwa kwa kuzingatia uwezo wa kifedha wa watumishi wa umma. Tumeendelea pia kushirikiana na taasisi za kifedha ili kuwawezesha wanunuzi kupata mikopo kwa masharti nafuu,” alisema Solomon.

Alisema ushirikiano huo na taasisi za fedha umeongeza fursa kwa wanunuzi wengi zaidi kumiliki nyumba kwa njia rahisi na ya uhakika.

Akifafanua zaidi kuhusu maendeleo ya mradi, Meneja wa Mradi huo, Mhandisi Yusuph Mlimakifu alisema kuwa hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 20 ya utekelezaji, huku kazi zikiendelea kwa kasi ili kukamilisha ujenzi kwa muda uliopangwa.

“Tunaendelea vizuri na kwa sasa hatujakumbwa na changamoto kubwa yoyote. Tunashukuru kwa usimamizi mzuri kutoka WHI na tunaahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kufanikisha mradi huu kwa kiwango bora,” alisema Mlimakifu.

WHI imeendelea kuwa kinara katika kusaidia sekta ya makazi nchini kwa kutekeleza miradi ya nyumba kwa watumishi wa umma katika mikoa mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki ya msingi ya kuishi kwenye makazi bora, salama na ya bei nafuu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img