12.9 C
New York

Kanisa la Shincheonji lakanusha Ripoti ya Le Parisien, ladai ni upotoshaji

Published:

Kanisa la Shincheonji la Yesu nchini Ufaransa limekanusha vikali taarifa iliyochapishwa na gazeti la Le Parisien Aprili 7, 2025, likiitaja kama yenye upendeleo, upotoshaji mkubwa wa ukweli na iliyodhalilisha jumuiya ya imani ya waumini wake.

Kupitia tamko rasmi lililotolewa Aprili 9, Kanisa hilo limesema kuwa ripoti hiyo iliegemea upande mmoja kwa kuhusisha kauli za wanachama wa zamani huku ikipuuza maelezo ya kina yaliyotolewa na uongozi wa kanisa. “Mistari miwili pekee” ndiyo iliyotolewa kwa majibu yao ya kina yaliyowasilishwa kwa mwandishi wa makala hiyo.

“Tulijibu maswali 12 ya mwandishi kwa maandishi yenye maelfu ya maneno, lakini ni sentensi mbili tu zilizotumika. Hii siyo tu dharau bali ni kizuizi kwa umma kupata taswira halisi ya Kanisa letu,” alisema msemaji wa Kanisa hilo.

Ripoti ya Le Parisien, iliyopewa kichwa “Walitutendea Kama Wanyama”, iliitaja Shincheonji kama mojawapo ya “makundi ya kiinjili yenye matatizo” nchini Ufaransa, ikiwatuhumu kwa kuwashinikiza waumini kushiriki kambi za mafunzo, kukatwa kwa mahusiano binafsi na kudaiwa fedha—madai ambayo kanisa limeyataja kuwa si ya kweli.

“Hiyo kauli ya ‘kututendea kama wanyama’ iliwashangaza na kuumiza waumini wetu. Haijawahi kutokea na haiwakilishi uhalisia wa maisha ndani ya Kanisa letu,” iliongeza taarifa hiyo.

Katika juhudi za kuonesha hali halisi, Kanisa hilo liliambatanisha ushuhuda wa waumini waliopo sasa, akiwemo Teresa (29) aliyesema:

“Kupitia Kanisa hili nimeelewa vyema maana ya kumtumikia Mungu na jinsi ya kuwa nuru duniani. Hakuna kulazimishwa, imani ni hiari.”
Axel (30), naye alisema:
“Imani hii imenipa maana ya maisha. Nimepata furaha, nimeweza kutimiza ndoto zangu, na hapa ndipo nilikutana na mke wangu.”

Tamko la Kanisa limeendelea kueleza kuwa baadhi ya picha zilizotumika kwenye ripoti hiyo zilitolewa nje ya muktadha sahihi, zikiwemo picha zilizodaiwa kuonesha adhabu ilhali zikiwa ni picha za utani zilizopigwa muda mrefu kabla ya tukio.

“Mtu aliyepo kwenye picha bado ni muumini, alipigwa picha hiyo kama utani, lakini ilitumika bila ridhaa yake, na sasa anapanga kufungua mashitaka,” ilisema taarifa hiyo.

Kuhusu madai ya udhibiti wa mahusiano au miongozo ya ndoa, Kanisa hilo limekanusha kabisa.

“Maamuzi ya ndoa ni ya hiari na yanatokana na imani ya mtu binafsi. Kutoa kauli kuwa kanisa linawalazimisha watu kuvunja mahusiano ni upotoshaji,” wamesema.

Pia Kanisa limeeleza kuwa mafunzo yaliyoitwa “kambi” yalikuwa ni programu fupi za kiroho zilizokuwa huru kushiriki na kuondoka, na tayari zimesitishwa kwa kuzingatia tafsiri tofauti zinazoweza kutolewa.

Mwisho wa taarifa yao, Shincheonji imeitaka Le Parisien na vyombo vya habari kwa ujumla kuheshimu maadili ya kitaaluma na dini, ikisema:

“Ripoti zenye upendeleo kuhusu dini zinachochea chuki na ubaguzi kwa waumini. Tunataka uandishi wa habari wa haki, unaojenga maridhiano na unaolinda haki za binadamu.”

Taarifa hiyo inasisitiza kuwa Kanisa la Shincheonji la Yesu limekuwa likifanya mawasiliano ya wazi na vyombo vya habari, na lipo tayari kupokea yeyote anayetaka kujionea kwa karibu maisha ya waumini wake ili kuondoa dhana potofu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img