12 C
New York

Urejelezwaji usio salama wa betri chakavu watajwa kuathiri mazingira na afya ya binadamu

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Imeelezwa kuwa urejelezwaji wa betri chakavu bila kuzingatia miongozo ya kimazingira ni chanzo kikubwa cha uchafuzi wa mazingira na huweza kusababisha madhara makubwa kwa afya ya binadamu kutokana na kemikali hatarishi hususan madini ya risasi yanayopatikana ndani ya betri hizo.

Kauli hiyo imetolewa Apeili 10, 2025 na Afisa Programu Mkuu wa Asasi ya AGENDA inayojihusisha na masuala ya mazingira na afya ya binadamu, Silvan Mng’anya, wakati wa warsha ya kujadili mwelekeo wa urejelezwaji wa betri chakavu iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Afisa Programu Mkuu wa Asasi ya AGENDA inayojihusisha na masuala ya mazingira na afya ya binadamu, Silvan Mng’anya akizungumza wakati wa warsha hiyo.

Mng’anya alisema iwapo urejelezwaji huo hautazingatia miongozo ya kimazingira, unahatarisha afya za watu wanaojihusisha moja kwa moja na shughuli hiyo, pamoja na wakazi wa maeneo yanayozunguka viwanda vya urejelezwaji.

“Madini ya risasi yanayopatikana katika betri na vifaa vya kielektroniki yana madhara makubwa kwa afya ya binadamu, yakiwemo kuathiri mfumo wa damu, uwezo wa kukumbuka, na mfumo wa fahamu,” alisema Mng’anya.

Aliwataka wamiliki wa viwanda vinavyojihusisha na urejelezwaji wa betri chakavu kufuata miongozo ya kitaifa na kimataifa, na kuwa tayari kupokea ushauri kutoka kwa mamlaka husika pindi wanapotakiwa kufanya maboresho ya mifumo yao.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mapitio ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mhandisi Luhuvilo Mwamila, alisema ipo haja ya kuwa na mwongozo wa pamoja utakaotumika kudhibiti taka za betri chakavu ambazo zimekuwa nyingi mitaani.

“Hivi sasa hakuna miongozo rasmi ya kushughulikia miradi ya aina hii. Tunayo miongozo ya jumla, lakini tunahitaji miongozo mahususi kwa betri zenye asidi ya risasi ili kudhibiti taka hizi kwa ufanisi zaidi,” alisema Mwamila.

Aliongeza kuwa katika mkutano wa hivi karibuni wa kikanda uliohusisha nchi za Afrika, nchi hizo ziliwasilisha hali ya urejelezwaji wa betri kwenye maeneo yao, na kubainika kuwa changamoto ni zinazofanana. Alipendekeza kuwepo kwa mwongozo wa pamoja wa kanda ili wawekezaji wa kigeni wafanye kazi kwa viwango vilivyo wazi na vinavyofanana.

Kwa upande wake, Mwanasheria wa NEMC, Angela Kileo, alieleza kuwa bado kuna uelewa mdogo miongoni mwa wadau kuhusu sheria zinazohusu usimamizi wa betri chakavu, jambo linalochangia uchafuzi wa mazingira.

“Sheria mama ya mazingira iko wazi na inaelekeza mtu anayeshughulika na taka hatarishi awe na vibali maalum, leseni, na TIN. Mtu anayeharibu mazingira anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema Kileo.

Aliongeza kuwa ongezeko la matumizi ya betri limechangia kuwepo kwa betri chakavu nyingi mitaani, hivyo ni muhimu wadau kuzitumia kama fursa za kiuchumi kwa njia salama zinazolinda afya na mazingira.

Naye Mratibu wa Shughuli kutoka Taasisi ya Waendesha Urejeleaji Taka Tanzania (TARA), Henry Kazula, alisema kwamba sera madhubuti na utekelezaji wake kwa vitendo ndio suluhisho la kuhakikisha mazingira salama na afya bora kwa wananchi.

Warsha hiyo iliandaliwa na AGENDA kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), na ilihusisha wadau kutoka sekta mbalimbali zinazojihusisha na mazingira na urejelezwaji wa taka ngumu kama betri za magari na zile za mifumo ya mawasiliano.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img