7.8 C
New York

DCEA ‘inavyotafuna mfupa’ wa dawa za kulevya nchini

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Katika juhudi za kuhakikisha Tanzania inakuwa salama dhidi ya athari za dawa za kulevya, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, inaendelea na operesheni kali za kukamata na kuteketeza dawa hizo haramu. Hatua hizi zinadhihirisha dhamira ya serikali kuhakikisha uzalishaji, biashara, na matumizi ya dawa za kulevya yanakomeshwa nchini.

Mnamo Februari 18, 2025, DCEA ilifanikiwa kuteketeza ekari 336 za mashamba ya bangi ndani ya Hifadhi ya Ikome wilayani Kondoa, mkoani Dodoma. Kilimo hicho haramu kilikuwa kimefichwa kwa kuchanganywa na mazao mengine halali ili kuzuia kugundulika. Katika operesheni hiyo pia, kilo 148 za mirungi zilinaswa.

Akizungumza katika operesheni hiyo, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kupambana na uhalifu wa dawa za kulevya.

“Hii ni operesheni kubwa ya kwanza kufanyika mkoani Dodoma. Inaonyesha kuwa kilimo cha bangi kimeanza kuenea katika baadhi ya maeneo ya mkoa huu. Tutaendelea kuchukua hatua kali kuhakikisha tunatokomeza kabisa uzalishaji na biashara ya dawa za kulevya,” alisema Lyimo.

Katika kipindi cha Januari hadi Februari 2025, DCEA kupitia ofisi zake za kanda imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 790.528 za dawa za kulevya katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Mbeya, Mtwara, na Dar es Salaam.

  • Dar es Salaam: Watuhumiwa watatu walikamatwa wakiwa na kilogramu 32.16 za bangi aina ya skanka, huku wengine wanne wakinaswa na kilogramu 5.1 za heroin na lita tano za kemikali aina ya Caffeine Anhydrous Pure, inayotumiwa kuongeza wingi wa dawa za kulevya.
  • Arusha: Kilogramu 98.55 za bangi, kilogramu 162.111 za mirungi, gramu 301 za heroin, gramu 195 za methadone, pembe moja ya ndovu, na risasi 11 za moto vilikamatwa. Pia, mtu mmoja alinaswa akiwa ameotesha miche ya bangi ndani ya nyumba yake kwa kutumia glasi za plastiki.
  • Kanda ya Ziwa – Wilaya ya Rorya, Mara: Hekari 24 za mashamba ya bangi ziliteketezwa, na watuhumiwa sita walikamatwa.
  • Kanda ya Pwani (Mtwara, Pwani, na Ruvuma): Kilogramu 322.201 za bangi, kete nane, na misokoto 216 ya bangi vilikamatwa. Pia, ekari nne za mashamba ya bangi ziliharibiwa na watuhumiwa wanane walikamatwa.
  • Kanda ya Nyanda za Juu Kusini – Mbeya: Kilogramu 21 za bangi zilinaswa, huku watuhumiwa 11 wakikamatwa.

Athari za uhalifu wa dawa za kulevya

Kamishna Lyimo alieleza kuwa uhalifu wa dawa za kulevya mara nyingi huambatana na uhalifu mwingine, ikiwemo biashara haramu ya silaha na ujangili wa wanyamapori.

“Tunaona pia ongezeko la uchakachuaji wa dawa za kulevya kwa kuchanganya kemikali ili kuongeza wingi wa dawa hizo, jambo linaloongoza madhara ya kiafya kwa watumiaji,” alisema Lyimo.

Serikali yataka ushirikiano wa wananchi

Kamishna Lyimo alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na DCEA kwa kutoa taarifa za siri kuhusu watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

“Kwa pamoja, tunaweza kulinda jamii yetu dhidi ya athari za dawa hizi hatari. Mamlaka inawahakikishia Watanzania kuwa tutaendelea kuvunja mitandao yote ya uhalifu wa dawa za kulevya kwa nguvu zote,” alisisitiza Lyimo.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Haubi, Fatina Ramadhani, alikiri kuwa baadhi ya wananchi katika eneo hilo wanajihusisha na kilimo cha bangi na akatoa wito wa kuachana na biashara hiyo haramu.

“Tunafanya mikutano ya kijamii kueleza madhara ya dawa hizi na pia tunaimarisha doria kwa kushirikiana na polisi jamii, askari wa akiba, na wahifadhi wa misitu,” alisema Fatina.

Wakazi wa Kondoa wapongeza juhudi za serikali

Mhifadhi wa Misitu, Amon Titus Mlimwa, akimwakilisha Meneja wa Wakala wa Huduma ya Misitu wilaya ya Kondoa, aliwashukuru wakazi wa Haubi kwa kujitolea kufyeka mashamba ya bangi.

“Misitu hii ni kwa faida yetu wenyewe. Tutaendelea na doria kila siku kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji na kata ili kuhakikisha tunatokomeza dawa za kulevya,” alisema Mlimwa.

Mkazi wa Mafai, Kata ya Haubi, Abushekhe Hamis Kalinga, alionyesha wasiwasi kuhusu athari za bangi kwa vijana, akisema wengi wameathirika.

“Wengine wanadai wanalima bangi kwa ajili ya pesa, lakini hasara ni kubwa kuliko faida. Tusipochukua hatua, kizazi kijacho kitakuwa na watoto wasio na akili timamu,” alisema Kalinga.

Vita dhidi ya dawa za kulevya inatuhitaji sote

Vita dhidi ya dawa za kulevya inahitaji juhudi za pamoja kati ya serikali, jamii, na vyombo vya usalama. Serikali kupitia DCEA imeonyesha dhamira ya dhati kuhakikisha kuwa uzalishaji na biashara ya dawa hizo zinadhibitiwa kwa nguvu zote.

Ni jukumu la kila Mtanzania kushirikiana na mamlaka husika katika kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na biashara hiyo haramu ili kuhakikisha nchi yetu inakuwa mahali salama kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img