11.3 C
New York

DCEA: Wanawake wateja wakubwa wa Skanka, wanatumia kupunguza mawazo

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Uchunguzi uliofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) umebaini kuwa wanawake ndiyo wateja wakubwa  wa dawa za kulevya aina ya skanka ikidaiwa kuwa  wanazitumia kupunguza msongo wa mawazo na kujistarehesha.

Hilo limebainika wakati wa operesheni iliyofanyika katika kipindi cha Oktoba na Novemba iliyowezesha kukamatwa kilo 687.32 za skanka na kilo moja ya hashishi katika eneo la Goba jijini Dar es Salaam zikiwa zimefichwa ndani ya nyumba ya mtuhumiwa.

Skanka ni jina la mtaani linaloitambulisha aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu (TetraHydroCannabinol – THC) ikilinganishwa na bangi ya kawaida.

Dawa hii ya kulevya hutokana na kilimo cha bangi mseto ambapo asilimia 75 ni bangi aina ya sativa na asilimia 25 ni bangi aina ya indica.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, akizungumza hivi karibuni Dar es Salaam alibainisha kuwa uchunguzi uliofanywa na mamlaka hiyo umebaini kuwa kuna ongezeko la matumizi ya dawa hizo za kulevya kufuatia udhibiti wa dawa zilizokuwa zikitumika hapo awali.

“Katika uchunguzi wetu ambao tulifanya kwenye vijiwe, saluni na maeneo mbalimbali tulibaini watumiaji wakubwa wa skanka ni wanawake. Kuna ambao tulizungumza nao na hata mimi binafsi nimezungumza na baadhi ya wanawake wanakiri kwamba wanatumia skanka kujiondolea mawazo.

“Ukisikiliza sababu zao wengi wanashindwa kuhimili misongo ya mawazo inayotonakana na changamoto za uhusiano hivyo wanakimbilia kwenye ulevi huo kwa kile wanachoamini inasaidia kupunguza mawazo,” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Hata hivyo Lyimo ameeleza kuwa tofauti na watumiaji hao wanavyoamini kwamba skanka inawapunguzia mawazo, uhalisia ni kwamba inawaingiza kwenye uraibu na hatari ya kupata changamoto ya afya ya akili.

Katika operesheni hiyo iliyofanyika kati ya Oktoba na Novemba zilikamatwa pia mililita 447 za dawa tiba zenye asili ya kulevya kati ya hizo mililita 327 zilikutwa nyumbani kwa mtuhumiwa eneo la Tabata Kinyerezi.

Mililita nyingine 120 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Codein zilikamatwa katika uwanaja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere zikiwa zinasafirishwa kwenda nje ya nchi.

“Dawa hizo ziliingizwa nchini kinyume na taratibu, zikiwa zimewekwa chapa bandia ya dawa za kuogeshea mbwa na paka ili kuepuka kubainika. Kukamatwa kwa dawa hizi ni ishara ya uwepo wa tatizo la matumizi holela ya dawa tiba zenye asili ya kulevya,”amesema.

Katika hatua nyingine mamlaka hiyo imewakamata watuhumiwa wawili  mkoani Dodoma wakiwa na granu 393 za dawa za kulevya aina ya heroin.

Watuhumiwa hao ni  Kimwaga Lazaro (37) na Suleiman Mbaruku (52) anayefahamika kama Nyanda akitajwa kuwa ni kinara wa biashara hiyo jijini Dodoma.

“Huyu Nyanda anafahamika kama kinara wa biashara ya dawa za kulevya jijini Dodoma, tumekuwa tukimfuatilia kwa muda mrefu na hatimaye tumefanikiwa kumkamata,”amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Kwa ujumla operesheni hiyo imefanikisha kukamatwa kilogramu 1,066.105 za dawa za kulevya, lita 19,804 za kemikali bashirifu, mililita 447 ya dawa tiba zenye asili ya kulevya na watuhumiwa 58.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img