2.6 C
New York

Shule ya Sekondari Mt. Joachim inavyoandaa vijana kwa maendeleo ya Taifa

Published:

Safina Sarwatt, Gazetini-Same

Mwaka 2013, Kanisa Katoliki Jimbo la Same lilianzisha shule ya sekondari ya wavulana, Mchepuo wa Sayansi ya Mtakatifu Joachim. Lengo kuu la kuanzishwa kwa shule hii ni kupanua wigo wa wataalamu wa masomo ya sayansi na kuleta mageuzi makubwa katika maendeleo ya Taifa.

Shule hii inakusudia kuwapa vijana wa Kitanzania elimu bora na malezi mazuri, huku ikiweka mkazo katika kukabiliana na upungufu wa watalamu wa sayansi, hasa katika kipindi ambacho Taifa linaelekea kwenye uchumi wa viwanda.

Katika mahojiano maalumu, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Same, Mhashamu Baba Askofu Rogate Kimaro, ameelezea hatua walizochukua kufanikisha maono haya. Akizungumza wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 10 ya shule, Askofu Kimaro amesema, “Wakati wa kuanzishwa kwa shule hii, tulikabiliwa na changamoto kadhaa, lakini tulifanikiwa kuzishinda kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu na nia thabiti ya kutoa huduma kwa jamii.”

Askofu Kimaro alikumbusha kuwa mwaka 2013 serikali ilitoa kibali cha usajili wa shule, na alishukuru kwa kuendelea kuziamini taasisi za dini. Aidha, alitaja msaada mkubwa kutoka serikali ya Italia, akisema, “Serikali za nchi za wenzetu huwa zinasaidia sekta binafsi; ni faraja kuona serikali inasaidia sekta hii.”

Aliongeza kuwa, “Taifa ambalo lina dira ya maendeleo ni lazima liwe na maono ya kuboresha huduma ya elimu ili iweze kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.”

Meneja Mkuu wa shule, Padre Deogratius Mchagi, alisema kuwa shule inafanya vizuri kutokana na uaminifu na jitihada zinazofanywa na uongozi wa shule. “Wanafunzi wengi wamejengewa uwezo mkubwa wa kujieleza na kujitegemea, yote hayo ni kutokana na uongozi makini,” alisisitiza.

Shule ina mazingira bora ya kufundishia, ikiwa na maabara za kisasa na maktaba yenye vitabu mbalimbali kwa wanafunzi kujisomea. Padre Mchagi alisema kuwa, “Tunatoa mafunzo ya vitendo, ambapo wanafunzi wanajifunza kutengeneza mabwawa ya samaki na kuandaa bustani za mboga mboga na matunda.”

Askofu Kimaro alitahadharisha kuhusu vijana wanaozurura bila kufanya kazi, akisema, “Kukataa kufanya kazi kunaweza kuleta kizazi cha vijana wasiojiweza.” Aliwakumbusha wazazi kutekeleza majukumu yao ya malezi ili kuandaa kizazi bora chenye maadili.

Katika shule hiyo, kila mwanafunzi anahimizwa kupanda miti, ambapo wameotesha miti zaidi ya 4000. Hii ni sehemu ya juhudi za utunzaji wa mazingira.

Mkuu wa shule, Charles Shogolo, alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2013, shule hiyo imewekeza katika kuwajenga watoto wa kiume wa Kitanzania ili kuongeza watalamu bora katika sekta ya sayansi. Alisema, “Shule yetu imekuwa na viwango vya juu katika ufaulu wa mitihani ya kitaifa, na mpango wetu ni kufuta daraja la tatu.”

Mwenyekiti wa bodi ya shule, Angella Kessy, alionyesha furaha kwa wazazi wanaowapeleka watoto wao katika shule hii. Alitoa wito kwa wazazi kuwa na muda wa kutosha kwa ajili ya malezi ya watoto, akisema, “Wazazi wanapaswa kutafakari walipoteleza na kuanza upya majukumu yao.”

Kwa ujumla, Shule ya Sekondari ya Sayansi ya Mtakatifu Joachim inaendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa vijana wa Kitanzania, ikijikita katika kutoa elimu bora na malezi yanayolingana na mahitaji ya wakati.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img