1.6 C
New York

Diwani kufunga kamera shule zote za kata yake kuimarisha usalama wa watoto

Published:

Na Grace Mwakalinga, Gazetini

DIWANI wa Kata ya Kiwira, wilayani Rungwe, mkoani Mbeya, Michael Mwamwimbe, ameanzisha utaratibu wa kufunga kamera za ulinzi za kielekroniki (CCTV), kwenye shule zote za Msingi zilizopo kwenye kata hiyo kwa ajili ya kuongeza ulinzi na usalama wa mtoto awapo shuleni ikiwa ni jitahada za kuhakikisha  wanalindwa dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kama vile mauaji, ubakaji na  ulawiti.

Mwamwimbe ameiambia GAZETINI kuwa utaratibu huo ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa ili kukabiliana na ukatili wa kijinsia kwa watoto shuleni.

Amesema ufungaji kamera za ulinzi za kielekroniki kwa majengo ya shule zote 12  za Msingi katika Kata hiyo  na kwamba ni wazo lake ambalo alitoa kwa  wananchi  ambao waliribariki  kwa ajili ya kuanza utekelezaji.

“Tumesikia  na kuona katika vyombo mbalimbali nchini vikiripoti juu ya vitendo vya ukatili aidha wakiwa shuleni au nyumbani, watoto wanabakwa, wanapigwa, wanauawa na kulawitiwa, sasa hii ni miongoni mwa njia itakayosaidia kukabiliana na vitendo hivyo,” amesema Mwamwimbe.

Ameongeza kuwa lengo lingine la kufunga kamera kwenye shule za Msingi ni kuongeza ulinzi na usalama wa mali za shule ambazo zimenunuliwa kwa fedha zinazotolewa na wananchi.

Amesema tayari shule ya Msingi Ilundo imefungwa kamera zenye thamani ya sh milioni 3.8  kwa ajili ya ulinzi wa vifaa vya kitaaluma zikiwemo mashine za kuchapisha karatasi za mitihani na kwamba sasa  wanahitaji kiasi cha  sh. milini 68 kwa ajili ya  shule 11 zilizobaki.

Amedai Kata ya Kiwira imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma ambapo kwa miaka minne mfululizo wameongoza kwa matokeo ya darasa la saba kiwilaya hivyo ni muhimu shule zikawekewe miundombinu rafiki  ili wanafunzi waendelee kufanya vyema  kwenye cckxmitihani yao.

Aidha, Diwani, Mwamwimbe amepongeza jitihada zinazofanywa na wananchi wa kata ya Kiwira kujitoa katika kuboresha miundombinu ya barabara, shule, soko na kilimo, ameahidi kushirikiana nao ili kata hiyo kuendelea kuwa ya mfano.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img