*Asema hayupo nchini kwa muda mrefu
*Awataka Watanzania kuwa makini na kupuuza taarifa hizo
Na Mwandishi Wetu, Gazetini
MFANYABIASHARA wa kimataifa, Rostam Azizi amesikitishwa na uwepo wa matapeli wa mitandao ya kijamii wanaosambaza taarifa za uongo zinazomhusisha na kuwekeza hisa katika Klabu ya Soka ya Yanga.
Rostam ametoa taarifa hiyo ya kusikitishwa na utapeli huo leo Oktoba 2, 2023 jijini Dar es Salaam huku hakisisitiza kuwa hajakutana na uongozi wa Yanga kama ilivyoelezwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya matapeli hao ambayo imemsababishia usumbufu mkubwa, Rostam mbaye pia ni Mwenyekiti wa kundi la makampuni ya Taifa (Taifa Group Ltd) anadaiwa kukutana na viongozi wa Yanga na kufikia nao makubaliano ya yeye kuwa tayari kuwekeza kiasi cha Sh bilioni 30 kama sehemu ya asilimia 49 ya hisa za mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.
Mbali na hilo, matapeli hao wa mtandaoni walikwenda mbele zaidi na kueleza kwamba, Rostam alikuwa amefikia makubaliano na Yanga kwa kuutaka uongozi wa klabu hiyo kutafuta wawekezaji wengine wawili zaidi ambao nao wangetoa kiasi cha Sh bilioni 20 kwa pamoja ili kukamilisha nakisi ya hisa asilimia 49.
“Katika hili, napenda kuwahakikishia wanachama na wapenzi wa timu ya Yanga na wapenda soka kwa ujumla ambao wamekuwa pia na dukuduku kubwa baada ya kusoma taarifa hizo potofu kuwa sijakutana na uongozi wa timu ya Yanga wakati wowote hivi karibuni kwani niko nje ya nchi kwa shughuli mahususi ya kifamilia kwa muda mrefu sasa.
“Hivyo napenda kuufahamisha umma wa Watanzania kutambua kuwa, kila wakati ninapokuwa na jambo linalogusa maslahi mapana ya nchi au uwekezaji nimekuwa nikijitokeza hadharani mimi mwenyewe au kwa kutoa taarifa rasmi inayotoka ofisini kwangu moja kwa moja.
“Kwa sababu hiyo basi, natoa wito kwa Watanzania kuwa makini na matapeli wa aina hiyo mitandaoni ikiwa ni pamoja na kuzipuuza taarifa za namna hiyo na natoa onyo kali kwa matepeli hao wa mitandaoni kukoma kutumia majina ya watu isivyopaswa,” ameeleza Rostam kupitia taarifa hiyo.