1.4 C
New York

‘Acheni kutumia chupa kunyonyesha watoto’

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini

Wataalamu wa lishe wameshauri akina mama wanaonyonyesha kuacha kutumia chupa zinazouzwa maduka ya dawa kunyonyeshea watoto kwani hatua hiyo inachochea watoto wengi kuacha kunyonya ziwa la mama kwa haraka.

Ushauri huo umetolewa Dar es Salaam leo Agosti 3, na Afisa Lishe Mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe nchini (TFNC), Wilbert Mgeni katika warsha ya kuwajengea uwezo wanahabari kuhusu wiki ya unyonyeshaji duniani inayoanza Agosti 1 hadi 7, kila mwaka.

Amesema mtoto anaponyonya maziwa kwa kupitia chupa zinazouzwa dukani zina mdomo mkubwa(chuchu) unaopitisha maziwa kwa wingi tofauti na ule wa ziwa la mama ambao hupitisha maziwa kidogo hatua ambayo inachochea mtoto kukinai kunyonya ziwa la mama.

“Unajua mtoto anapokuwa ananyonya ziwa la mama maziwa yanatoka taratibu hatua inayomlazimu kuvuta, lakini anaponyonyeshwa kwa kutumia chupa zinazouzwa dukani hizi chuchu zake zinanjia kubwa ambazo zinaruhusu maziwa kutoka kwa wingi na kwa urahisi.

“Lakini anavyorudi kwenye ziwa la mama anakuta kwamba maziwa yanatoka kidogo tofauti na kule kwenye chupa, hivyo inamlazimu kutumia nguvu kubwa kuyavuta jambo linalomsababisha kukinai ziwa la mama mapema,”amesema Mgeni na kuongeza kuwa ni bora maziwa ya mama yakakamuliwa na kuwekwa kwenye kikombe badala ya kutumia chupa hizo.

Upande wake Afisa Lishe kutoka TFNC, Gelagisa Gwarasa akizungumzia changamoto ya watoto kuacha kunyonya mapema maziwa ya mama amesema sababu nyingine ni harufu inayosabaishwa na mabadiliko ya manukato yanayopakwa na akina mama wanaonyonyesha.

“Sababu nyingine inayochochea watoto kukataa kunyonya ziwa la mama mapema ni harufu ya mama, unakutaka kwamba mtoto alikuwa amezoea harufu ya mama baada ya muda mama akabadili mafuta hii ni sababu nyingine ambayo inasabisha watoto wengi kuacha kunyonya kwani harufu ya mama inakuwa inamsumbua.

“Sambamba na hayo, jambo jingine ni kwamba kama mama atakuwa amekunywa au kumeza dawa inakuwa inasabisha kwamba mtoto ananyonya maziwa yenye harufu ya dawa, hivyo kukacha maziwa hayo,” amesema Gwarasa.

Mama afanye nini?

Wataalamu hao wameshauri kuwa iwapo hali hiyo ya mtoto kukataa kunyonya inapojitokeza, kwanza mama hapaswi kuacha kumnyonyesha na kutumia njia mbadala, badala yake anapaswa kufika kituo cha afya kwa ajili ya kupata ushauri wa wataalamu.

“Siyo suluhisho kwamba mtoto akigoma kunyonya mara moja tu basi mama na wewe unaridhika hapana, anachopaswa kufanya kama mama ni kumpeleka mtoto huyo kwenye kituo cha afya kwa ajili ya kufanyiwa uchuguzi huenda akawa anavidonda mdomoni, au kunachangamoto ya kiafya tumboni, hivyo kuwahi kumkatisha mtoto kunyonya punde tu anapokataa kunyonya siyo suluhisho,” amesema Mgeni.

Awali, akifungua warsha hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TFNC, Germana Leyna ameitaja kaulimbiu ya mwaka huu 2023 kuwa ni ‘Saidia unyionyeshaji, wezesha wazazi kule watoto na kufanya kazi zao za kila siku‘ huku akiwakumbusha akina mama na akina baba kutimiza jukumu lao.

“Wiki hii ni wiki ya kukumbushana ni kwanini maziwa ya mama ni muhimu katika mstakabali wa mtoto na kwani huu ndiyo mtaji wa kwanza kabisa wa mama kumpatia mwanae sambamba na baba ambaye ana wajibu wa kutekeleza jukumu lake muhimu la kuhakikisha kwamba mama anapata lishe bora ili aweze kumnyonyesha mtoto vizuri.

“Kwa hiyo kaulimbinu ya mwaka huu inalenga kuhakikisha kwamba kama wanajamii tunatambua jukumu hili la mama na kumsaidia ili aweze kupata mtoto mwenye afya bora, tunakumbushana namna ambavyo jamii inaweza kuainisha majukumu ya kulea watoto hasa unyonyeshaji pamoja na shughuli za uzalishaji mali hasa kwa huyu mama kwani miaka ya hivi karibuni mama anaanza kurudi kutafuta kwa haraka zaidi tofauti na kipindi cha nyuma.

“Pia kuweka mazingira wezeshi ya unyonyeshaji mahali pa kazi sambamba na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ili kweka mazingira mazuri ya unyonyeshaji maziwa ya mama mahala pa kazi,” amesema Leyna.

Mkurugenzi Mkuu wa TFNC, Germana Leyna(kushoto) akizungumza katika warsha hiyo.

Akitaja stahiki anazostahili mama mwajiriwa anayejifungua mtoto ana haki ya kupata likizo ya siku 84 iwapo amejifungua mtoto mmoja na siku 100 iwapo amejifungua watoto zaidi ya mmoja huku baba akipata likizo ya siku tatu katika wiki ya kwanza.

“Changamoto iliyopo katika kutekeleza utaratibu huu ni wanawake wengi kufanya kazi katika sekta isiyo rasmi na hivyo kushindwa kunufaika na utaratibu huu, hivyo ni jukumu la wanajamii wote kuhakikisha kwamba mama anapata nafasi ya kumnyonyesha mtoto kikamilifu,” amesema Leyna.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img