1.4 C
New York

GGML: Tupo tayari kushirikiana na TANESCO

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imesema ipo tayari kushirikiana kikamilifu na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kwa kutumia umeme gridi ya Taifa baada ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme na mradi wa kupeleka umeme katika migodi ya kampuni hiyo kukamilika.

Pia, imeipongeza Tanesco na wizara ya nishati kwa kuja na mpango mkakati wa miaka 10 ambao utaliwezesha shirika hilo kuanzisha vyanzo vipya vya nishati endelevu kwani ni jambo litakalolisaidia Taifa kutimiza lengo namba saba la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) linalozungumzia matumizi ya nishati inayofikika, ya gharama nafuu, endelevu na ya kisasa kwa wananchi wake.

Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayeshughulikia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo akichangia mjadala wa nishati kupitia Jukwaa la fikra la Mwananchi uliofanyika juzi jijini Dar es Salaam. Wengine ni washiriki wa mjadala huo ulioenda sambamba na uzinduzi wa mpango mkakati wa miaka 10 wa Tanesco.

Hayo yameelezwa jana na Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayeshughulikia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo wakati akichangia mjadala wa nishati kupitia Jukwaa la fikra la Mwananchi.

Shayo alisema mpango huo mkakati wa miaka 10, utaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kusini mwa nchi za Jangwa la Sahara kutimiza lengo hilo la maendeleo endelevu (SDGs)

“Ni hatua kubwa kwa Tanesco kutafsiri kwenye mkakati wake lile lengo namba saba,” alisema.

Alisema licha ya kwamba kampuni nyingi za madini tangu miaka ya 2000 hutumia umeme wanaouzalisha wenyewe, sasa Serikali imekuwa na jitihada za makusudi kufungamanisha sekta ya nishati na sekta kubwa za uzalishaji kwa kuzalisha umeme unaotosheleza mahitaji ya wawekezaji wakubwa.

“Sisi kwa sekta ya madini tunaona hii kama ni baraka kubwa kwa sababu huwezi kuendesha migodi mikubwa kama ya kwetu (GGML) kwa kutumia jenereta,” alisema.

Alitoa mfano kuwa GGML hutumia Megawati 29 ambazo huzalisha kwa mafuta lakini sasa wanatamani kuona mradi wa kupeleka umeme wa Tanesco katika mgodi wa kampuni hiyo ukikamilika ili kupunguza gharama za uendeshaji.

“Tukijiunga tu na Tanesco kwenye gridi ya Taifa na kutoka kwenye umeme tunaouzalisha wenyewe, tutapunguza gharama za umeme kwa asilimia 50, tuta-save dola za Marekani milioni 19 kila mwaka. Pia tutapunguza hewa ya ukaa kilotons 81 kufikia 2030,” alisema.

Alisema kwa kuwa nchi ipo katika mipango ya kuwekeza pakubwa katika sekta ya madini kwa kuanzisha migodi ya uzalishaji wa madini mengine sehemu mbalimbali nchini, ni Dhahiri kuwa Tanesco itafanikiwa kuongeza mapato makubwa kutokana na mchango wa migodi hiyo kwenye matumizi ya umeme.

Alisema Tanesco wanajenga laini ya kilovolt 220 kutoka Bulyanhulu hadi Geita kisha laini ya kilomita sita yenye kilovolt 33 kuelekea katika mgodi wa GGML ilihali kampuni hiyi ikijenga kituo cha kupoza umeme kwenda kilovolt 11 kwa gharama ya dola za Marekani milioni 24.4.

Awali akizindua mpango huo mkakati wa Tanesco, Waziri wa Nishati, Januari Makamba aliwataka wananchi wawe na subira wakati Shirika hilo linafanya mageuzi ya utendaji kazi wake.

Alisema Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuipa mtaji TANESCO ili itekeleze mipango yake kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wananchi na Afrika kwa ujumla.

Naye Mkurugenzi wa TANESCO, Maharage Chande alisema shirika hilo linakusudia kuendelea na mipango yake ya kuboresha huduma kwa wateja wake, kupitia miradi mbalimbali ikiwemo wa kufua umeme katika Bwawa la Julius Nyerere, ambao unatarajia kuanza kuzalisha umeme Juni 2024.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img