10.2 C
New York

Makala| Rehema: Mwanangu alifariki sababu ya utoto wangu-1

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

“Mwanangu wa kwanza alifariki dunia wakati nikijifungua, madaktari waliniambia kuwa njia yangu ya uzazi ilikuwa ndogo. Nilikuwa na miaka 17 tu kwa wakati huo….”

Hii ni sehemu ya maneno yanayohusu ya safari ya maisha aliyoipitia na anayoendelea kuyapitia binti wa miaka 26, ambaye kwa sasa ni mama wa watoto wawili baada ya mwanaye wa kwanza kutangulia mbele za haki.

Mama huyu ambaye katika makala haya tumembatiza jina la Rehema Zabroni, anasema maisha ni magumu na hatamani tena kuendelea kuishi kwenye uhusiano wa mume na mke ambao amedumu nao kwa miaka kadhaa sasa.

“Natamani kutoka katika hii ndoa isiyo na furaha lakini kinachoniweka hapa ni watoto wangu wawili. Sitamani tena kuzaa mwingine. Nasubiri hawa wakue niachane kabisa na huyu mwanaume kwani amekuwa mtu wa vitisho tu kwangu,” anasema Rehema na kuongeza:

“Najuta sana kwani sasa ningekuwa hata daktari wa Watoto, kazi ambayo niliitaman sana. Ningefika huko kama ningeendelea kuvumilia kazi ngumu na manyanyaso niliyokuwa nayapitia wakati nikiishi kwa kwa Shangazi yangu.”

Rehema ambaye kwa sura anaonekana kusononeka kutokana na maisha anayoishi na mume wake, ni wa pili kuzaliwa kati ya watoto sita wa mama yake, Stela Ngailo (48) ambaye alizaa na wanaume tofauti.

Kwa mujibu wa Rehema, baba yake anafahamika kwa jina la Zabron Sanga na anasema uchungu wa maisha yake ulianza mwaka 2004 akiwa na umri wa miaka minane. Anasema wakati huo walikuwa wakiishi katika kitongoji cha Lupila kilichoko Njombe (wakati huo ikiwa Wilaya ndani ya Mkoa wa Iringa). Kwa sasa Njombe ni mkoa unaojitegemea.

“Hapo tayari nami nilikuwa na mdogo wangu wa miaka miwili na mama yangu alikuwa mjamzito. Ila kila mmoja wetu, alikuwa na baba yake. Hali ya maisha yetu haikuwa ya kuridhisha kwani tulikuwa tunaishi na mama tu,” anasema Rehema.

Rehema anasema ili kutoa nafasi ya matunzo kwa wadogo zake, alilazimika kwenda kuishi kwa mjomba wake anayemtaja kwa jina moja la Jasanga, katika kijiji cha Ikonda wilayani Makete.

“Nilikwenda kwa mjomba ambaye pia alikuwa akiishi na mke wake (shangazi) yangu. Walezi wangu hawa wote hawakuwa na mtoto, hivyo mimi ndiyo nilikuwa mtoto pekee katika familia hii.

“Maisha yaliendelea na kwa siku za mwanzo nilikuwa nikipatiwa mahitaji muhimu kwani tayari nilikuwa nimeshaandikishwa kuanza shule (elimu ya msingi),” anasimulia Rehema.

Haikuwa rahisi

Rehema anasema changamoto zilianza akiwa darasa la tatu kwani hapo alilazimika kwenda shamba kulima, pamoja na kushughulika na mifugo; ng’ombe na mbuzi. Pia alianza kufanya vibarua vya kusomba matofali.

“Hiyo ilikuwa ni baada ya mjomba kuniambia kuwa nilitakiwa nijifunze kujitegemea kwa kufanya kazi mbalimbali kutokana kwamba kwetu tulikuwa maskini, hivyo nilivumilia changamoto hizo nikamaliza darasa la saba.

“Bahati nzuri matokeo yalipotoka nilichaguliwa kujiunga na shule ya Sekondari ya Lupalilo,” anasema Rehema. Hata hivyo, safari ya masomo ya Rehema haikudumu kutokana na kushindwa kumudu ada ya shule.

“Wakati huo serikali ilikuwa bado haijaondoa ada shuleni, hivyo tulikuwa tukilipa Sh 20,000. Muhula wa kwanza mjomba alinilipia Sh10,000 lakini mhula wa pili alikataa kwa kile alichosema kwamba sikufanya kazi kwa bidii wakati wa likizo, hivyo akanitaka nitafute fedha ili nijilipie pamoja na michango mingine.

“Nilienda shuleni bila ada lakini nikarudishwa. Nilivyorudi kumwambia mjomba akaniambia natakiwa kufanya kazi kwa bidii mara mbili zaidi ili niweze kupata hiyo fedha, jambo ambalo lilinishinda,” anasema Rehema.

Uamuzi wa kutoroka

Rehema anasema kutokana na changamoto hiyo aliamua kuchukua uamuzi wa kutoroka na kurudi kwa mama yake kwa lengo la kutaka kumuuliza ni wapi alipo baba yake.

“Baada ya kufika na kumuuliza, alinieleza baba yangu ni nani na alikuwa wapi kwa wakati huo. Nilichukua jukumu la kumtafuta baba yangu lakini nilichokikuta sikukitarajia kwani baba ndiye ilikuwa mwanzo wa mimi kuolewa katika umri mdogo.

“Kwanza baba alinikubali kama mwanaye na kunirejesha shule iliyokuwa jirani kwa jili ya kuendelea na masomo, lakini niliacha shule sababu ya mateso kutoka kwa mama wa kambo,” anasema Rehema.

Anasema kutokana na manyanyaso ya mama wa kambo alianza kupoteza mwelekeo wa masomo kwani alikuwa akipigwa na kunyimwa chakula, hatua liyosababisha aache shule akiwa kidato cha kwanza.

“Nilitoroka na kwenda Njombe mjini kwa kumdanganya mwenye gari kuwa mama yangu atakuwa stendi na ndiye atalipa nauli. Baada ya kufika stendi wakati kondakta akishusha mizigo ya abiria wengine, nilikimbia bila kuniona,” anasema.

Safari ya ndoa

Rehema anasema akiwa Njombe aliingia kwenye moja ya nyumba zilizokuwa eneo la mjini kwa lengo la kuomba msaada.

“Niliomba kazi za ndani na bahati nzuri nilikubaliwa ila sikuwa nalipwa mshahara, badala yake nilipewa vyakula na zawadi ndogo ndogo kutokana kwamba nami sikuwa na sehemu ya kwenda. Halafu kwa umri wangu mdogo sikujua kama nilikuwa nanyimwa stahiki zangu.

“Nilifanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja, baadaye yule mama ambaye ni bosi wangu akatokea kunipenda kutokana na ufanyaji kazi wangu, hivyo akanitaka niolewe na kijana wake, wakati huo nilkuwa sijui hata maana ya ndoa. 

Anasema baada yakukubali ombi hilo, mabosi wake hao walimwambia kuwa walihitaji kufika kwa wazazi wake, hivyo aliwapeleka kwa mama yake.

“Baada ya kufika walimpatia mama zawadi na wao wakaeleza hitaji lao, na wakakubali niolewe kwa mahari ya Sh500,000 fedha ambayo walilipa siku hiyohiyo. Baadaye tulirejea nyumbani na nikaanza kuandaliwa kuwa mke.

Nilidhani ndoa ni kuishi tu vizuri, nikakubali,” anasema Rehema ambaye kwa wakati huo alikuwa na miaka 16. Hii inamaanisha kwamba binti huyu aliingia kwenye ndoa akiwa bado mtoto. Kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Mtoto ya waka 2009 kinasomeka: “Tafsiri ya “mtoto” 4.-(1)…. “Mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka kumi na nane atajulikama kama mtoto”.

Mwaka 2021 Benki ya Benki ya Dunia ilitoa ripoti ikibainishas kuwa zaidi ya wasichana 120,000 huacha shule kila mwaka nchini Tanzania na kati ya hao 6,500 ni kwa sababu ya ujauzito au kuwa na watoto.

Kama hiyo haitoshi ripoti nyingine ya benki hiyo kuhusu Tathimini ya Ukatili wa Kijinsia Tanzania (Tanzania Gender Based Violence Assessment) iliyozinduliwa Aprili 5, 2022 inabainisha kuwa msichana mmoja kati ya watatu aliolewa kabla ya kufikia miaka 18.

Kadhalika takwimu za Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya (TDHS) hapa nchini za 2015-2016 zilionyesha kuwa asilimia 36 ya mabinti wenye miaka 20 hadi 24 waliolewa kabla hawajatimiza umri wa miaka 18. Kwa mujibu wa wachambuzi wa takwimu hizo, maana yake ni kwamba kwa wastani, wasichana wawili kati ya watano huolewa kabla hawajatimiza umri wa miaka 18. 

Tafiti mbalimbali zinabainisha kuwa ndoa za utotoni ni pale binti au msichana anapoolewa na mwanaume mwenye umri mkubwa, hali ambayo husababisha msichana husika kukosa nguvu pale unapotokea unyanyasaji dhidi yake.

Pia ipo tafsiri nyingine inayosema ndoa za utotoni “Ni muungano wa jadi, dini au usiyo rasmi ambapo amabibi au bwana harusi anakuwa na umri chini ya miaka 18, mara nyingi msichana huwa mdogo akiolewa na mwanaume mtu mzima au mzee,”.

Wakati Rahema akizaiwa mwaka 1998, tayari mumewe alikuwa na umri wa miaka 19. Hivyo basi hivi sasa mwanamke akiwa na umri wa miaka 26, mumewe ana miaka 43.

Utafiti wa Demografia ya Afya nchini (TDHS) wa mwaka 2010 unaitaja mikoa yenye viwango vikubwa vya ndoa za utotoni na viwango vya asilimia kwenye mabano kuwa ni Shinyanga (59), Tabora (58), Mara (55) na Dodoma (51). 

Ripoti mpya iliyotolewa Aprili 2022 na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) inabainisha kuwa ndoa za umri mdogo na mimba za utotoni ziliongezeka wakati wa janga la Uviko-19.

“Kupitia uchunguzi wa vyombo vya habari na ufuatiliaji wa haki za binadamu, LHRC ina kumbukumbu 37 za matukio ya ndoa za utotoni, mbili zaidi ya zile zilizoandikwa mwaka 2020,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo na kuongeza:

“Wasichana wengi waliofunga ndoa za utotoni walikuwa katika kundi la umri wa miaka 13 hadi miaka 16.” Kwa amujibu wa LHRC matukio mengi yaliripotiwa katika mikoa ya Katavi, Shinyanga, Mara, Mtwara, Lindi, Kilimanjaro, Dodoma, Kigoma na Rukwa.

Takwimu Muhimu za Msingi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI za mwaka 2020, zinaeleza kuwa idadi ya wasichana wanaacha shule iliongezeka kutokana na ujauzito iliongezeka kutoka 3,439 mwaka 2015 hadi 5,398 mwaka 2019.

Ujauzito wa kwanza

Rehema anasema baada ya kuingia kwenye ndoa kwa mtindo huo, baadaye alipata ujauzito akiwa na umri wa miaka 17.

“Hata hivyo mtoto wangu wa kwanza alifariki dunia nilipokuwa najifungua. Madaktari waliniambia kuwa njia yangu ya uzazi ilikuwa ndogo sababu nilikuwa na umri mdogo wa miaka 17 tu kwa wakati huo. 

“Kwa sasa nina watoto wawili ambao mmoja nilijifungua kawaida nikiwa na miaka 20 na mwingine kwa njia ya upasuaji, hivyo nimelazimika kukubaliana na hali halisi licha ya ukweli kwamba inaniuma sana kuona ndoto zangu hazijatimia maana nilitamani kuwa daktari bingwa wa watoto,” anasema Rehema ambaye kwa sasa anaishai jijini Dar es Salaam na mume wake huyo.

Ripoti ya matokeo ya utafiti unaoitwa ‘Ndoa za utotoni Tanzania’ iliyotolewa Machi 2, 2017 inasema wasichana wanaoingia katika ndoa mapema pia hupata ujauzito mapema, hali ambayo huwaweka katika hatari zaidi wakati wa ujauzito na kujifungua

“Kwa mfano, wakinamama kati ya umri wa miaka 15 na 19 wanao uwezekano wa kufariki mara mibili zaidi ikilinganishwa na wakinamama ambao wenye umri kati ya miaka 20 na 24,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo iliyotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jami, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na taasisi kadhaa zikiwamo Plan, CDF, Forward na UNFPA…Inaendelea

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img