1.4 C
New York

Visual| Tunayofahamu kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali 2022/2023

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba amewasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha wa 2022/2023.

Dk. Nchemba amewasilisha bajeti hiyo leo Jumanne Juni 14, 2022 bungeni jijini Dodoma ambapo inaonesha kuwa jumla ya Sh Trilioni 41.48 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika.

Katika fedha hizo jumla ya mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 28.02, sawa na asilimia 67.5 ya bajeti yote.

Aidha, kati ya mapato hayo, mapato yatakayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) yanakadiriwa kuwa Sh trilioni 23.65 na mapato yasiyo ya kodi (Wizara, Idara, Taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa) yanakadiriwa kuwa Sh trilioni 4.37.

“Misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo inatarajiwa kuwa Sh trilioni 4.65, sawa na asilimia 11.2 ya bajeti yote. Aidha, Serikali inatarajia kukopa Sh trilioni 5.78 kutoka soko la ndani ambapo Sh trilioni 3.30 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na kiasi cha Sh trilioni 2.48 ni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

“Vilevile,serikali inatarajia kukopa Sh trilioni 3.03 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara kwa lengo la kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” amesema Dk. Mwigulu.

Amesema, katika mwaka 2022/23, serikali inapanga kutumia jumla ya Sh trilioni 41.48 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo.

Kati ya kiasi hicho, Sh trilioni Sh 26.48 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwa ni asilimia 63.8 ya bajeti yote, ikijumuisha Sh trilioni 11.31 kwa ajili ya ulipaji wa deni la serikali na gharama nyingine za Mfuko Mkuu na Sh trilioni 9.83 kwa ajili ya mishahara ikiwemo nyongeza ya mshahara, upandishaji wa madaraja kwa watumishi na ajira mpya.

“Aidha, Sh trilioni 5.34 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC) ikijumuisha Sh bilioni 200.0 kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya watumishi na wazabuni.

“Matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 15.0, sawa na silimia 36.2 ya bajeti yote. Kati ya kiasi hicho, Sh trilioni 12.31 ni fedha za ndani, sawa na asilimia 82.0 ya bajeti ya maendeleo na Sh trilioni 2.70 ni fedha za nje,” amesema Dk. Nchemba.

Amefafanua zaidi kuwa fedha za maendeleo za ndani zinajumuisha: Sh trilioni 1.11 kwa ajili ya kugharamia mradi wa ujenzi wa reli kwa kiwango cha Standard Gauge; Sh trilioni 1.44 kwa ajili ya kugharamia mradi wa kufua umeme wa Maji wa Julius Nyerere; Sh trilioni 1.18 kwa ajili ya Mfuko wa Barabara.

“Sh bilioni 944.1 ni kwa ajili ya mifuko ya Reli, Maji na REA; Sh bilioni 570 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; Sh bilioni 230.0 kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya madeni yaliyohakikiwa ya wakandarasi; na Sh bilioni 346.5 kwa ajili ya kugharamia elimumsingi bila ada,” amesema Dk. Nchemba.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img