HIVI karibuni, bilionea mwenye jina kubwa nchini China, Sun Dawu, alifikwa na hukumu nzito ya miaka 18 gerezani.
Mbali ya kifungo, kampuni yake imelazimishwa kulipa faini ya Dola za Marekani milioni 4.6.
Sun alishukiwa na hukumu hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuhamasisha uvunjifu wa amani.
Achilia yeye, pia watoto wake wawili, sambamba na kaka zake wawili walikumbana na kifungo cha kati ya miezi 18 hadi 12.
Sun ni nani?
Akiwa na umri wa miaka 67 kwa sasa, Sun ni mmoja kati ya wafanyabiashara matajiri China, akijihusisha na bidhaa za kilimo na ufugaji kupitia kampuni yake ya Dawu Agricultural and Animal Husbandry Group iliyoajiri watu zaidi ya 9,000.
Huku akiwa na utajiri wa kutosha, bado Sun ameendelea kulima na wakati mwingine viongozi wa Serikali walikuwa wakimfuata kumwomba ushahuri wa namna ya kuinua kipato cha wakazi wa vijijini.
Tatizo lake na Serikali
Kwa miaka mingi, Sun amekuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali ya China, hasa sare zake kwa maeneo ya vijijini.
Mara zote huwa akiishinikiza Serikali kupunguza kodi kwa wakulima, sambamba na kuwapatia mikopo ya kuwezesha shughuli zao.
Mwaka 2003, alishitakiwa kwa kile kilichosemekana kuwa ni kuchangisha fedha kinyume cha kufuata utaratibu wa kuomba kibali cha Benki Kuu.
Katika hilo, alihukumiwa kifungo cha miaka minne gerezani lakini Serikali ililazimika kufuta hukumu baada ya wanaharakati na raia kuchachamaa.
Si tu kilimo, pia wakati mwingine ungemkuta Sun akikosoa ukandamizwaji wa haki za binadamu nchini China.
Mwaka 2015, Sun aliunga mkono bila hofu wanasheria na wanaharakati zaidi ya 300 waliokuwa wanashikiliwa na vyombo vya dola.
Usikilizaji wa kesi hii iliyompeleka rumande umechukua takribani wiki mbili, huku ikifuatiliwa kwa karibu na jumuhiya za kimataifa.
Kwanini hukumu hii inakosolewa?
Kama ilivyotarajiwa na wengi, wanasheria wake wameipinga hukumu hiyo, pia wakiahidi kukata rufaa.
Hata kabla ya hukumu, wanasheria wake walitilia shaka namna waendesha mashitaka walivyokusanya ushahidi.
Hoja yao ni kwamba ushahidi uliokusanywa wakati mtuhumiwa (Sun) akiwa ameshikiliwa unapaswa kutotumika kwa kuwa ulipatikana kwa njia za kutesa watu.
Naye mwanasheria Wang Yu anasema hukumu nzito aliyoshushiwa Sun ni kielelezo cha China isiyojali uhuru wa kujieleza.
Hali ikoje kwa wakosoaji wa Serikali?
Kwa miaka ya hivi karibuni, Serikali ya China imekuwa makini dhidi ya wakosoaji.
Mathalan, mwanasheria na mwanaharakati maarufu nchini humo, Xu Zhiyong, amekuwa kizuizini tangu Februari, mwaka jana.
Hatua ya kushikiliwa ilikuja baada ya Xu kuchapisha barua ya wazi iliyomtaka Rais wa nchi hiyo, Xi Jinping, aachie madaraka.
Ni kama ilivyowahi kumtokea bilionea Ren Zhiqiang, ambaye kwa tabia yake ya kukosoa Serikali alijikuta akihukumiwa kifungo cha miaka 18 gerezani baada ya kuhusishwa na tuhuma za rushwa.
Hatima ya matajiri ikoje?
Kutokana na namna China inavyofilisi kampuni za matajiri wanaoikosoa Serikali, wataalamu wa uchumi wanaiona hatari kubwa.
Mfano, kwa mwezi huu pekee, utajiri wa mmiliki wa mtandao wa kijamii wa Tencent, Pony Ma, uliporomoka kutoka Dola bilioni 60 hadi chini ya Dola bilioni 50.
Wakati hali hiyo ikimkuta pia mmiliki kampuni maarufu ya Alibaba, Jack Ma, inaelezwa kwamba matajiri wengine wanapoteza hadhi ya kuitwa mabilionea kwa kuwa wanafilisiwa na Serikali.
China inarudi ilikotoka?
Kipindi fulani katika historia ya China, kuwa tajiri kuliko wengine ilionekana kuwa ni hatari kwa kuwa kila ‘jicho baya’ lingekutazama.
Hata hivyo, mambo yalibadilika mwaka 1978 baada ya rais wa wakati huo, Deng Xiaoping, kusema China ingepiga hatua kiuchumi endapo watu wake wangepewa uwanja wa kushindana kuwa matajiri.
Kwa kile kilichotokea kwa Sun, ni wazi sasa China imerudi kwenye enzi zile, kwamba kuwa tajiri ni hatari na badala yake uchumi ushikwe na Serikali.