1.6 C
New York

Uchambuzi|Huyu ndiye aliyemng’oa madarakani Edgar Lungu

Published:

HATIMAYE Tume ya Uchaguzi ya Zambia imemaliza kazi yake ya msingi, kumtangaza mshindi wa kinyang’anyiro cha urais, hatua iliyochukua siku tatu za kuhesabu kura.

Mgombea wa upinzani kupitia Chama cha United Party for National Development (UPND), Hakainde Hichilema, ndiye aliyeibuka kidedea mbele ya rais aliyekuwa akiwania awamu yake ya pili madarakani akiwakilisha Chama cha Patriotic Front (PF), Edgar Lungu.

Itakumbukwa kuwa Hichilema mwenye umri wa miaka 59 aliungwa mkono na vyama 10 chini ya mwamvuli wa UPND, mara ya kwanza kabisa kuiona Zambia ikiwa na nguvu kubwa zaidi ya upinzani.

Katika matokeo yaliyotangazwa, kura milioni saba zilipigwa katika majimbo 156 na kisha Hichilema akajikusanyia asilimia 60 (2,810,777) huku mpinzani wake, Lungu, akiambulia asilimia 38 (1,814,201).

Kwa kuwa hiyo ni tofauti ya kura zaidi ya milioni moja, basi Hichilema hatalazimika kuingia kwenye uchaguzi wa marudio kwa kuwa amezidi asilimia 50.1 ya kura kama inavyotakiwa na Katiba.

Licha ya malalamiko ya Lungu mwenye umri wa miaka 64, akisema uchaguzi uligubikwa na figisu, hii ilikuwa mara ya sita kwa Hichilema kuingia kwenye mbio za kuifukuzia nafasi ya kuingia Ikulu.

Wasifu wa Hichilema

Hichilema anatokea familia ya kimasikini, mara kadhaa akisimulia alivyotembea pekupeku kwenda shule, pia akisema hata chuo kikuu alikosomea masuala ya Fedha na Biashara alifika kwa msaada wa Serikali.

Katika siasa, tajiri huyo wa biashara ya ufugaji wa ng’ombe, alichomoza zaidi mwaka 2006, alipochaguliwa kuwa rais wa Chama cha UPND baada ya kifo cha aliyekuwa akishikilia wadhifa huo, Anderson Mazoka.

Kipindi hicho, akagombea kiti cha urais akiwakilisha muungano wa vyama vitatu uliofahamika kwa jina la United Democratic Alliance (UDA). Itakumbukwa, aliungwa mkono na aliyekuwa rais wa zamani wa Zambia, Kenneth Kaunda, ingawa alibwagwa na Michael Sata wa Chama cha Patriotic Front (PF).

Cha kukumbukwa zaidi kutoka kwake ni kile kilichotokea mwaka 2014, ambapo alijitokeza hadharani kupinga vikali kuwa yeye si mfuasi wa Freemason, madai yaliyokuwa yameibuliwa na Mchungaji wa Kanisa la Orthodox, Edward Chomba.

Hata hivyo, mwaka 2017 ulikuwa mbaya kwake alishikiliwa na vyombo vya dola kwa madai ya kuratibu mipango ya kuipindua Serikali. Haikuwa hivyo tu, pia alishutumiwa kwa kosa la uhaini. Katika hilo la uhaini, ilisemekana Hichilema alihatarisha maisha ya Rais Lungu kwa kitendo cha msafara wake kukataa kupisha ule wa kiongozi huyo.

Kitendo cha Hichilema kukamatwa kililaaniwa vikali na jumuhiya za kimataifa, hata kuzua maandamano katika nchi za Afrika Kusini na Uingereza, achilia mbali yale yaliyofanyika Zambia. Hatimaye, alikaa jela miezi minne.

Katika mahojiano yake juu ya maisha ya jela, Hichilema alisema zilikuwapo jitihada za kuuliwa kwani alifungiwa chumba cha peke yake kwa siku nane, ambapo hakupata chakula, maji, wala mwanga.

Safari ya kibabe Ikulu

Katika uchaguzi wa kwanza kushiriki, yaani mwaka 2006, Hichilema aliambulia asilimia 25 ya kura zote na kushika nafasi ya tatu nyuma ya Michael Sata (29.37%) na mshindi Levy Mwanawasa (42.98%).

Mwaka 2008, alijitosa tena na safari hii alipata asilimia 19.7 na kushika nafasi hiyo hiyo alipochuana na Michael Sata (38.64) na mshindi Rupiah Banda (40.63).

Uchaguzi wa mwaka 2011 ulimshuhudia Hichilema akichuana tena na wawili hao na hakukuwa na mabadiliko, alishika nafasi hiyo hiyo ya tatu, akijikusanyia asilimia 18.54 ya kura.

Sasa, mambo yalianza kubadilika katika Uchaguzi wa mwaka 2015 kwani alishika nafasi ya pili kwa asilimia 47 ya kura, akizidiwa kidogo tu na Lungu (48.84%).

Hichilema aliendeleza ushindani mkali mbele ya Lungu. Ifahamike, Lungu alipata ushindi akiwa na asilimia 50.35, wakati Hichilema alikuwa na asilimia 47.63.

Kipi kilichomponza Lungu?

Kwa miaka yake sita aliyokaa madarakani kuwaongoza raia milioni 18 wa Zambia, Lungu alikumbana na ukosolewaji mkubwa. Mathalan, alipondwa kwa namna alivyoshindwa kusimamia haki za ubinadamu.

Ni kama alivyonyooshewa kidole katika ishu za kushindwa kudhibiti vitendo vya rushwa, achilia mbali mdororo wa uchumi na uhaba wa ajira. Juu ya hilo la uchumi, unaizungumzia Zambia yenye deni la nje linalofikia Dola za Marekani bilioni 12.

Changamoto nyingine inayoweza kuwa chanzo cha ‘kura za hasira’ walizopiga raia kumng’oa Lungu ni kushuka kwa bei ya madini ya shaba, achilia mbali thamani ya fedha yao, Kwacha, kushuka kwa asilimia 40.

Hata utafiti uliofanywa miezi kadhaa kabla ya Uchaguzi Mkuu huo, ulionesha wazi kwamba ni asilimia 23 tu ya wapigaji kura walikuwa tayari kuchagua Chama tawala, PF.

Lungu atakwenda Mahakamani?

Kama ilivyodokezwa hapo juu, Lungu haoni kama haki ilitendeka katika Uchaguzi huo uliomwondoa madarakani. Kwa waliofuatilia uchaguzi huo, watakumbuka malalamiko yake yalianza hata kabla ya matokeo.

Kwa mujibu wa kile alichosema Lungu, uchaguzi wa safari hii, tofauti na ule wa mwaka 2016 aliomgaragaza Hichilema, uligubikwa na vurugu nyingi, hasa kwenye maeneo ambayo upinzani ulikuwa na ushawishi mkubwa.

Aidha, Lungu anadai kuwa katika baadhi ya maeneo ilishuhudiwa mawakala wa chama chake wakishambuliwa, sambamba na kufukuzwa kwenye vituo vya kuupiga kura.

Kile kilicho wazi kwenye Katiba ni kwamba Lungu anaweza kupeleka kilio chake kwenye Mahakama ya Katiba. Hata hivyo, hatua hiyo inatakiwa kuchukuliwa ndani ya siku saba tangu mshindi alipotangazwa.

Waangalizi wa kimataifa wanasemaje?

Kwa upande wao, Uchaguzi haukuwa na dosari za kuufanya upoteze haki ya kupata mshindi. Hata hivyo, wanakosoa namna janga la Corona lilivyotumiwa na chama tawala, Chama cha Patriotic Front.

Katika hilo, wanatolea mfano kitendo cha vyombo vya dola kumzuia mgombea wa upinzani, Hichilema, kuingia kwenye baadhi ya maeneo kwa madai ya mikusanyiko inaweza kurahisisha maambukizi ya virusi vya Corona.

Juu ya madai ya Lungu, wasomi wa siasa wanaamini anajaribu kutumia kile alichofanya Donald Trump, ambaye alianza kukosoa uchaguzi kabla ya kushindwa kwa kuwa alishaona ufiny wa nafasi ya kurudi Ikulu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img