Wakati sheria ya ongezeko la tozo za miamala ya simu iliyoanza kutumika nchini Julai 15, mwaka huu, ikilalamikiwa kila kona, Watanzania walio wengi wameanza kutaja huduma za kibenki kama kimbilio lao katika kutuma na kupokea fedha.
Wengi wanairudia njia hiyo ya benki baada ya awali kutoipa kipaumbele kutokana na umaarufu na urahisi wa matumizi ya simu katika kuiwezesha miamala ya fedha katika maeneo ya mijini na vijijini.
Awali, kwa mujibu wa watumiaji wa huduma hizo za kifedha kwa njia ya simu walisema huduma hiyo ilikuwa bora zaidi na nafuu katika kufanikisha mahitaji ya kutuma na kupokea kiwango cha wastani wa fedha ambacho ni Sh 1,000 hadi Sh milioni 10 za Tanzania.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka huu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), watumiaji wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi walikuwa milioni 32.7 kufikia Machi, mwaka huu (robo ya kwanza ya mwaka), ikiwa ni ongezeko kutoka milioni 32.5 waliokuwapo Januari, mwaka huu. Hilo ni sawa na ongezeko la watumiaji 298,346 (asilimia 0.9) ndani ya kipindi cha miezi mitatu, huku idadi hiyo ikipanda kila mwezi.
Aidha, watumiaji wa huduma za kibenki nao wamekuwa wakiongezeka kwa kasi. Mfano, Desemba mwaka jana, kulikuwa na akaunti za simu-benki (mobile money subscribers) milioni 32.26 zilizokuwa zimeongezeka kwa kasi kutoka akaunti milioni 31.1 zilizokuwapo mwishoni mwa Oktoba, 2020.
Wadau wa masuala ya uchumi na fedha wanaeleza kuwa takwimu hizo zinadhihirisha kuwa Watanzania wengi wanazidi kufikiwa na huduma za kifedha na kuchangia katika ukuaji wa uchumi kwa kuiwezesha Serikali kupata mapato.
Katika takwimu hizo za TCRA zilizotolewa wiki hii, zinabainisha kuwa asilimia 88 ya watumiaji wote wa huduma za kifedha kwa njia za simu wanatumia kampuni za Vodacom (M-Pesa), Tigo (Tigo Pesa), na Airtel (Airtel Money).
Ni kwa maana hiyo basi, kampuni tatu zilizosalia, yaani Zantel (Eazy Pesa), Halotel (Halopesa) na TTCL (TTCL Pesa) zinagawana asilimia 12 ya watumiaji hao wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi.
Katika mchuano huo, M-pesa ndiyo inayotawala soko nchini baada ya kuweza kurekodi watumiaji milioni 13.6, sawa na asilimia 42 ya soko zima, ikifuatiwa na Tigo Pesa (asilimia 26) na Airtel Money ikiwa na asilimia 20.
Mvuto wa njia hiyo ya miamala ya fedha kupitia simu ni namna inatajwa kuokoa muda na kupunguza gharama zisizo za lazima kwa watumaji na wapokeaji. Mathalan, wengi walikuwa wakikerwa na misululu mirefu wanayokutana nayo kwenye benki mbalimbali nchini, hasa kwenye miji mikubwa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na Dodoma.
Hata hivyo, Watanzania wengi kwa sasa waona ni vema zaidi kukamilisha miamala kwa njia ya benki ili kuokoa kiwango kikubwa kilichotambulishwa kwenye tozo za Serikali.
Kwa mujibu wa Takwimu za Umiliki wa Akaunti za Benki zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika Ripoti yake ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi mwaka 2017/18, asilimia 12.3 ya kaya Tanzania Bara ndizo zilizokuwa na walau mtu mmoja mwenye akaunti ya benki.
Vilevile, ripoti hiyo inaonesha kuwa wananchi wenye akaunti za benki ni wengi (asilimia 23.8) maeneo ya mjiji kuliko vijijini (asilimia 6.1). “Kaya zenye wanakaya wenye akaunti benki zinatofautiana kimkoa, kuanzia asilimia 2.3 kwa Mkoa wa Kigoma hadi asilimia 31.4 kwa Mkoa wa Dar es Salaam,” inabainisha ripoti hiyo.
Pia, ripoti hiyo inaonesha umiliki wa akaunti ya benki kwa kaya ambayo mkuu wake ni mwanaume ni ni asilimia 13.5, huku ambazo hakuna mwenye akaunti ikiwa ni asilimia 86.5. Kwa upande wa kaya ambazo mkuu wake ni mwanamke, wenye akaunti ya benki ni asilimia 9.4, wakati wasionazo ni asilimia 90.6. Hii ni sawa na kusema kwamba kaya ambayo mkuu wake mwanaume zina kiwango cha juu ya umiliki wa akaunti za benki, ikilinganishwa na zile ambazo mkuu wake ni mwanamke.
Wakati huo huo, ripoti ikabainisha kwamba Dar es Salaam ndiyo kinara katika orodha ya mikoa yenye wamiliki wa akaunti za benki (asilimia 31.3), huku mkoa wa mwisho ukiwa na asilimia 2.3 tu.