18.6 C
New York

Rais Samia mgeni rasmi Tuzo za ‘Samia Kalamu Awards’

Published:

Na Esther Mnyika, Gazetini

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa tuzo za wanahabari zinazojulikana kama Samia Kalamu Awards, zenye lengo la kuchochea uandishi wa habari za maendeleo katika nyanja mbalimbali nchini.

Tuzo hizo zimeandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa ushirikiano na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na zinatarajiwa kutolewa Aprili 29, 2025 katika ukumbi wa Mabele, Mabeyo Complex jijini Dodoma.

Akizungumza Aprili 15, 2025 jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk. Rose Reuben amesema tuzo hizo zimekusudiwa kuhamasisha uandishi wa habari unaojikita kwenye utafiti wa kina, uchambuzi makini, uzingatiaji wa maadili ya taaluma na maudhui ya ndani yenye kuakisi maendeleo ya taifa.

“Tuzo hizi zimechagizwa na mafunzo ya mwaka 2024 yaliyolenga kuendeleza uandishi wa habari za maendeleo. Zinalenga pia kukuza uzalendo na kujenga taswira chanya ya nchi,” amesema Dk. Reuben.

Kwa mujibu wake, tuzo hizo zimegawanywa katika makundi matatu:

Tuzo Maalumu za Kitaifa:

Hizi ni pamoja na Tuzo ya Chombo cha Habari Mahiri Kitaifa, Tuzo ya Wanahabari Wabobevu, Ofisa Habari Mahiri wa Serikali, Mwandishi Bora Kitaifa, na Tuzo ya Uandishi wa Habari kuhusu Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Tuzo kwa Vyombo vya Habari:

Hili ni kundi linalojumuisha televisheni, redio za kitaifa na kijamii, magazeti na vyombo vya habari mtandaoni.

Tuzo za Kisekta
Zitahusisha waandishi waliobobea katika sekta mbalimbali kama afya, maji, nishati, mazingira, jinsia na makundi maalumu, ujenzi, biashara, maliasili, utalii, mifugo, uvuvi, uchumi wa buluu, kilimo, sanaa, utamaduni, michezo, Tehama, ardhi, madini, elimu, fedha na uwekezaji.

Dk. Reuben ameongeza kuwa tukio hilo litarushwa mubashara kupitia televisheni, redio na mitandao ya kijamii ili kuruhusu wananchi kushuhudia na kushiriki kwa njia ya mtandao, hasa wale waliopiga kura kwa waandishi na vyombo vya habari vilivyoteuliwa.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img