Na Ramadhan Hassan, Gazetini-Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, amesema kuwa uhamisho ni haki ya kila mtumishi wa umma, lakini akasisitiza kuwa waajiri wanapaswa kutumia hekima na busara wanapotekeleza mchakato huo.
Akizungumza leo Aprili 17, 2025 jijini Dodoma na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Waziri Simbachawene alisema mtumishi anaruhusiwa kuomba uhamisho baada ya kutimiza angalau miaka mitatu ya kazi.

“Unakuta mwingine ni mgonjwa na anahitaji huduma za matibabu sehemu nyingine, basi uhamisho wake ni wa lazima. Hili ni jambo linalohitaji busara kubwa kutoka kwa waajiri,” alisema Simbachawene.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo alifafanua kuwa kupandishwa cheo si haki ya moja kwa moja bali kunatokana na utendaji kazi wa mtumishi husika. Alieleza kuwa mtumishi anapaswa kujituma na kuonyesha ufanisi kazini ili kustahili kupanda daraja.
Akizungumzia nidhamu ya kazi na mahudhurio, Waziri Simbachawene alisema Serikali kwa sasa imeweka mfumo rasmi wa mahudhurio katika ofisi zote za umma ili kufuatilia kwa karibu muda wa kuingia na kutoka kwa watumishi.
“Siku hizi hakuna kwenda kazini halafu unaanza na chai. Kila mtumishi anatakiwa kufuata ratiba rasmi ya kazi na kuweka alama ya mahudhurio kwa mfumo uliowekwa,” alisisitiza.
Aidha, alitoa onyo kali kwa watumishi wanaoghushi vyeti, akisema kuwa Serikali imeazimia kukomesha kabisa tabia hiyo na kwamba sheria zitachukua mkondo wake kwa wote watakaobainika kufanya udanganyifu huo.
“Hii ni moja ya kesi mbaya sana katika utumishi wa umma. Tunalifanyia kazi kwa nguvu zote na hatutasita kuchukua hatua kali kwa wanaobainika kughushi,” alionya Simbachawene.
Waziri huyo amesisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha huduma za umma zinaboreshwa na watumishi wanatekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia maadili ya kazi.