2.6 C
New York

TPC Moshi yaboresha elimu kupitia ufadhili na miundombinu ya kisasa

Published:

Na Safina Sarwatt, Moshi

Zaidi ya wanafunzi 1,000 kutoka familia zenye mazingira duni wamefaidika na mpango wa ufadhili wa masomo ulioanzishwa na Kiwanda cha Sukari TPC Moshi kupitia taasisi yake ya Foundation for Community Transformation in Kilimanjaro (FTK). Tangu kuanzishwa mwaka 2012, mpango huu umewezesha wanafunzi kutoka maeneo yanayozunguka kiwanda hicho kuendelea na masomo yao ya elimu ya juu.

Kwa mujibu wa Msimamizi wa FTK, Lazaro Urio, kiwanda cha TPC hutenga zaidi ya Shilingi milioni 400 kila mwaka kufadhili masomo ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita kwenda vyuo vya ufundi na vyuo vikuu. Mpango huu unalenga kupunguza changamoto za kifedha zinazowazuia wanafunzi kuendelea na masomo.

“Mpango huu ni sehemu ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) wa TPC, ambapo tunalenga kubadilisha maisha ya wanafunzi na kupunguza pengo la kielimu katika jamii,” alisema Urio.

Miundombinu ya Kisasa kwa Maendeleo ya Elimu

Mbali na ufadhili wa masomo, FTK imewekeza katika kuboresha miundombinu ya elimu kwa maeneo yanayozunguka kiwanda. Hivi karibuni, taasisi hiyo imekamilisha ujenzi wa bweni jipya lenye uwezo wa kuhifadhi wanafunzi 68 wa kike katika Shule ya Sekondari ya TPC kwa gharama ya Shilingi milioni 147.

Bweni hilo limekuwa mkombozi kwa wanafunzi waliokuwa wakilazimika kutembea umbali wa kilometa 14 hadi 20 kwenda na kurudi shuleni kila siku, hali iliyokuwa ikiwakosesha muda wa masomo na kuwaweka katika mazingira hatarishi.

“Changamoto ya umbali iliwafanya wanafunzi, hususan wa kike, kuchelewa kufika shuleni na kukosa vipindi muhimu. Uwekezaji huu unatoa fursa kwao kujikita zaidi katika masomo,” alieleza Urio.

Shule hiyo pia imeboreshwa kwa ujenzi wa maktaba ya kisasa yenye maabara ya kompyuta kwa gharama ya Shilingi milioni 126. Maktaba hiyo inaweza kuhudumia wanafunzi 48 kwa wakati mmoja, ingawa bado inahitaji Shilingi milioni 25 kukamilisha mahitaji ya thamani.

“Natoa wito kwa wadau mbalimbali kuungana nasi kuhakikisha maktaba hii inapata vifaa muhimu vitakavyowezesha wanafunzi kupata elimu bora zaidi,” alisema Urio.

Manufaa kwa Jamii na Wanafunzi

Kwa mwaka, TPC hutenga zaidi ya Shilingi bilioni 1.5 kupitia FTK kwa ajili ya miradi ya kijamii inayohusisha elimu, afya, na maendeleo ya kiuchumi kwa zaidi ya watu 95,000 wa Moshi Vijijini na Simanjiro, Manyara. Huduma hizi zinachangia kupunguza umaskini, kuongeza viwango vya elimu, na kutoa fursa kwa vijana kufanikisha ndoto zao za kitaaluma.

Gladines Kimaro, mmoja wa wanafunzi walionufaika, alieleza jinsi mpango huu umebadilisha maisha yao.

“Kabla ya bweni, tulilazimika kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni, hali iliyokuwa inachosha na kutufanya tukose vipindi. Leo hii tuna nafasi ya kujifunza kwa utulivu na kufikia malengo yetu,” alisema Kimaro.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya TPC, Salehe Shaban, alibainisha kuwa bweni hilo limechangia kupunguza utoro na kuongeza viwango vya ufaulu, hasa kwa watoto wa kike.

Sekta Binafsi Kama Mshirika wa Maendeleo

Mpango wa TPC Moshi kupitia FTK ni mfano bora wa jinsi sekta binafsi inaweza kuchangia maendeleo ya kijamii. Ufadhili wa masomo na uboreshaji wa miundombinu ya elimu si tu vinainua viwango vya elimu, bali pia vinachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa jamii zinazozunguka kiwanda.

Hatua hizi zinaonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na jamii katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kuinua maisha ya watu wengi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img