Na ,wandishi Wetu, Gazetini
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde ametembelea banda la Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) katika maonesho ya sita ya teknolojia ya madini Geita na kupata maelezo kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa.
Waziri huyo pia alishuhudia mfano wa mradi wa uwanja wa kisasa wa michezo (Magogo Stadium) unaojengwa na GGML kwa lengo la kuendeleza michezo mkoani Geita.
Akipata maelezo kutoka kwa Meneja Mawasiliano wa GGML, Stephen Mhando alielezwa kwamba kampuni hiyo ambayo imeshiriki mara zote sita tangu maonesho hayo yaasisiwe mwaka 2018, imekuwa mdhamini mkuu na mwaka huu pia imetoa Sh milioni 150.
Mhando alimueleza pia Waziri kuwa mbali na udhamini huo mwaka huu, GGML imetoa jenereta maalumu ili kukabiliana na dharura yoyote ya umeme itakapojitokeza.
Mbali na Mavunde kutembelea idara tisa za GGML zilizopo katika maonesho hayo, pia Mhando alimueleza kuwa zaidi ya Sh bilioni 2.4 hadi sasa zimetumika katika mradi huo wa ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo.
“Kazi hii inaendelea na sisi GGML kama wadhamini wakuu wa Timu ya Geita Footbal Club, tunaamini kuwa uwanja utakapokamilika utakuwa moja ya chanzo cha mapato hata kwa halmashauri ya Geita,” amesema.