Na Faraja Masinde, Gazetini
“Nilipata maambukizi ya VVU nikiwa na miaka 24, baada ya kupata mwanaume mwenye pesa sana lakini kumbe alikuwa na maambukizi, ndugu zangu walinitenga nakuniambia ‘wewe huna lolote la kusema unasubiri siku ya kufa tu, usitwambie kitu chochote’ nilitengewa hadi vyombo, mama alilia sana,” Mwamvita.
Hiyo ni sehemu ya simulizi ya Mwamvita Masai(36 sio jina lake halisi) mama wa watoto wawili ambaye alipata maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI(VVU) akiwa na umri wa miaka 24 baada ya kuangukia kwenye penzi la mwanaume mwenye maambukizi ya VVU zaidi ya miaka 12 iliyopita.
Maisha mazuri yalivyompa VVU
Kwa maneno yake mwenyewe, Mwamvita ambaye anaishi katika moja ya vitongoji vinavyounda Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera nchini Tanzania, anasema kuwa tamaa yake ya kutaka kuyafanikisha maisha mazuri kwa haraka ikiwamo kupangishiwa nyumba ndiyo iliyomsukuma kupata maambukizi ya VVU.
“Nilipata maambukizi ya VVU nikiwa na miaka 24, kifupi nilikuwa bado ni binti mdogo, nilipata mwanaume mwenye pesa sana ambaye nilianza nae mahusiano akanipangishia chumba tukawa tunaishi kama mume na mke mjini Bukoba lakini nyumba ndogo.
“Alikuwa akinunua vitu vya lishe sana nyumbani na alikuwa akikuta sijapika vyakula hivyo vya lishe anaanza kunigombeza, tulikuwa tukikaa au muda mwingine tukitoka matembezini ananiambia kuwa alimfumania mke wake na mtu aliyekuwa akimhisi ana maambukizi ya UKIMWI kwamba lakini mkewe huyo alipopima akakuta yuko salama,” anasema Mwamvita.
Mwamvita anasema kuwa hapo ndipo ulikuwa mwanzo wa mashaka yake juu ya mwenzi wake huyo, kivipi…
“Mashaka yangu yalianzia hapo, kwanza nilijiuliza kwanini akikuta sijatayarisha vyakula vya lishe ananigombeza? lakini nikaunganisha pia tukio lakumfumania mke wake na mtu mwenye VVU nikasema hapana lazima twende tukapime, lakini akagoma.
“Baada ya kukataa niliamua kwenda mtaani nikatafuta kituo cha afya nikapima virusi vya Ukimwi,” anasema.
Mama huyo wa watoto wawili anafafanua zaidi kuwa isivyobahati alikutwa ana maambukizi ya VVU, nakwamba ilibidi ajikaze sana ili watu wasiweze kumgundua.
“Sababu wakati wakutoka nje kulikuwa na watu wengi sana, hivyo nililazimika kujikaza kwani majibu yangu yalikuwa yameambatana na barua yakwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando(ya jijini Mwanza) kwa ajili ya kuunganishwa kwenye huduma ya dawa, hivyo nililazimika kuficha barua ile,” anasema Mwamvita.
Safari yake haikuwa nyepesi
Mwamvita anasema baada ya kupokea majibu hayo alienda moja kwa moja nyumbani kwa mpenzi wake mwingine (Mwanaume wa pili) mbali na yule aliyemsadiki kumwambukiza VVU, nakumsihi kwenda kupima.
“Nikaenda na mimi pia nilikuwa na mchepuko mwingine nikapata ujasiri wakumwambia akapime VVU, bahati nzuri alipima akakutwa hana maambukizi kabisa.
“Lakini mume wangu niliyekuwa naishi naye yeye hakutaka kabisa kusikia suala la kwenda kupima hatua ambayo ilinilazimu niachane naye. Miaka mitatu baadaye nilipata ujauzito kwa mwanaume mwingine kabisa nje ya wale wawili(watatu) sikumweleza hali yangu, tulifanikiwa kupata mtoto wa kike ambaye alikuwa salama kutokana kwamba nilizingatia maelekezo ya wataalamu wa afya,” anasema Mwamvita.
Hata hivyo, safari ya Mwamvita haikuishia hapo, kwani wakati akiendelea na maisha alifanikiwa kupata mwanaume mwingine(wanne), ambaye huyo ndiye anasema ni chaguo la moyo wake na kwa sasa anatambulika hadi nyumbani kwao.
“Katika kuendelea na maisha ndipo nikapata mwanaume wa kunioa moja kwa moja ambaye tulikutana kwenye kazi za ushauri kwani na yeye anaishi wa maambukizi ya VVU.
“Mume wangu huyu ndiye anatambulika hadi nyumbani kwani alikwenda kujitambulisha na tumebahatika kupata mtoto mmoja ambaye yuko salama kabisa kwani tulizingatia matumizi sahihi ya dawa za kupunguza makali ya VVU(ARV).
“Kwa hiyo, hadi sasa watoto wetu wako vizuri na maisha yetu yako vizuri, nimekuwa muwazi, najikubali nauwezo wa kusimama sehemu yoyote ile nakutangaza afya yangu kwa sababu nilishajikubali na nimeona kuwa na maambukizi ya VVU siyo mwisho wa maisha.
“Pia hata ambaye hana maambukizi ya VVU wote tunafanana hatuna tofauti hata ukitusimamisha huwezi kusema huyu ana maambukizi na yule hana, hapana,” anasema Mwamvita.
Familia ilivyomuweka kando
Kwa mujibu wa Mwamvita, baadhi ya ndugu zake walimnyanyapaa ikiwamo kumtengea vyombo vya kutumia huku wengine wakipuuza hata mawazo yake kwenye vikao huku wengine wakienda mbali zaidi kwa kumpa jina la marehemu mtarajiwa.
“Kwanza kabisa nilianza kuwambia ndugu kabla sijamwambia baba na mama, walininyanyapaa sana wakanitengea vyombo vya chakula na vitu vingine ya kutumia kwa kile walichoamini kwamba ningeweza kuwaambukiza, kw akweli hali ile ilinitesa sana.
“Kama hiyo haitoshi, tulikuwa tukiingia kwenye vikao vya ukoo labda ukichangia hoja mtu anakwambia ‘wewe huna lolote la kusema unasubiri siku ya kufa tu, usitwambie kitu chochote.
“Hali ile iliniumiza sana kiasi kwamba kama nisingepiga moyo konde, basi kwa sasa ningekuwa nimebakiza jina tu duniani labda na watoto wangu wawili,” anasema Mwamvita ambaye kwa sasa ni Mjasiriamali na kuongeza kuwa:
“Mwaka 2015 ulipofika wakati wa kumwachisha mwanangu kunyonya ikabidi nimwambie mama ukweli.
“Mama alilia sana, ikabidi nimwambie asilie, nilimwambia hili ni jambo la kawaida mbona nina karibu miaka saba nyuma, nikamuuliza ‘kwani nisingekwambia ungejua’, akasema hapana, nikamwambia basi jikaze hili ni suala la kawaida, kuanzia hapo akawa anachukulia ni jambo la kawaida huku ndugu zangu wao wakiendelea kunitenga kama walivyoazimia tangu awali,” anasema Mwamvita.
Hata hivyo licha ya kupitia wakati huo mgumu, Mwamvita anasema kuwa hakuwahi kuonyesha unyonge mbele ya ndugu zake hao, badala yake alibaki na maumivu yake moyoni.
Haikuwa kazi nyepesi kukabiliana na ile hali lakini nilisema Mwenyezi Mungu kwa kuwa ulinipitisha kwenye hili, basi naamini utanipa uvumilivu na ujasiri.
“Kweli siku zilienda, baadaye nadhani mama alikutana na wanafamilia wale na kuwaeleza hali nakwamba kile kilikuwa ni kitu cha kawaida tu, sababu baadae walianza kubadili mtazamo wao huku wengine wakinieleza kuwa ‘tulijua ungekufa muda wowote, kumbe unaweza kuendelea kuishi iwapo utatumia dawa’ kwa kweli niliwapa somo ambalo lilibaki msaada kwa kila mmoja aliyelipata.
“Hivyo, hata sasahivi wale waliokuwa wananiambia mimi nasubiri tarehe ya kufa tu sasahivi wananichukulia kawaida tu kama mtu mwingine, kwa hiyo nina amani hata zawadi zinakuja, wapo wanaoniletea matunda na vitu vingine,” anasema Mwamvita.
Hali ilivyo kuhusu Unyanyapaa
Wakati Mwamvita akibaina aina hiyo ya unyanyapaa, matokeo ya Utafiti wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania(TACAIDS) kuhusu unyanyapaa kwa WAVIU Tanzania Bara uliofanyika kati ya Februari na Septemba 2021 ukilenga kutathmini kiwango cha unyanyapaa na ubaguzi kwa WAVIU nchini unaonyesha kuwa, kitaifa unyanyapaa umepungua kutoka asilimia 28.0 mwaka 2013 hadi asilimia 5.5 mwaka 2021.
Utafiti wa mwaka 2013
Awali, katika utafiti wa kwanza uliofanywa na TACAIDS mwaka 2013 ukihusisha mikoa mitano ya Dar es Salaam, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro na Iringa, matokeo yake yalibainisha kuwa asilimia 13.8 ya WAVIU walihisi wenye hatia kwa kuwa na VVU.
Aidha, asilimia 29.8 ya WAVIU walihisi aibu kuwa na VVU huku asilimia 42.9 ya WAVIU walijiona hawana thamani kutokana na kuwa na kuishi na VVU.
Mbali na hayo, unyanyapaa binafsi ulikuwa asilimia 20.5 huku ule wa ndani ya jamii ulikuwa asilimia 28.
Utafiti wa mwaka 2021
Katika matokeo ya utafiti wa mwaka jana yaliyotolewa na Tacaids mwaka huu hali inaonyesha kuwa asilimia 51.0 ya WAVIU walifichua hali zao kwa watu wao wa karibu (kama wenzi, familia, marafiki wa karibu) huku asilimia 46.0 walipata usaidizi kutoka kwa watu waliokuwa karibu nao walipotambua kuhusu hali yao ya VVU.
Aidha, asilimia 2.4 ulikuwa ni unyanyapaa kutoka kwa mikusanyiko ya kijamii au shughuli huku asilimia 1.3 ikiwa ni unyanyapaa kutoka katika shughuli za Kidini au mahali pa Ibada.
Pia unyanyapaa kutoka kwenye shughuli za familia ilikuwa ni asilimia 2.4 huku ule wa vitendo vya matamshi ya kibaguzi au porojo ukiwa ni asilimia 8.9.
Kwa mujibu wa utafiti huo mikoa kinara pamoja na viwango vyake kwenya mabano ni pamoja na Kilimanjaro(19.5%), Tanga(10.5%) ikifuatiwa na mikoa ya Mbeya(2.8) na Iringa(1.4%).
Hii ni sawa na kusema kwamba kama nchi imepiga hatua kubwa kwani jamii imeendelea kuwa na akina Mwamvita wengi ambao wamekuwa ni sehemu ya waelimishaji juu ya maambukizi ya VVU hivyo elimu imezidi kuenea zaidi ikilinganishwa na miaka ya nyuma wakati Mwamvita na watu wengine wanapata maambukizi.
Pia mwamko wa vyombo vya habari katika kuelimisha umma juu ya masuala mbalimbali yanayohusu UKIMWI umekuwa mkubwa jambo ambalo TACAIDS na wadau mbalimbali wakiwamo UN-WOMEN wanapaswa kupongezwa.
Kwa nini ni muhimu kudhibiti unyanyapaa
Jacob Kayombo ni Mratibu wa Programu zinazohusu masuala ya Ukimwi na Saratani kwa Wanawake katika Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wanwake (UN WOMEN) ambaye anasema kuwa mwarobani wa kufikia ndoto ya 0 ifikapo 2030 ni kubadili mitazamo.
“Tunapenda kuona jamii ikibadilisha mtazamo wa kijamii kuhusu mila na desturi, kwani kwa muda mrefu unyanyapaa na mila hatarishi au zisizofaa vimekuwa vikiongelewa katika lugha ambayo tunadhani vinahusu watu waloiko vijijini sana jambo ambalo siyo kweli.
“Mfano tumeona masuala kama unyanyapaa ambayo kwa huko nyuma tulidhani kuwa yanatajwa kwenye maeneo machache sana ya VVU na Ukimwi, lakini kumbe ni kinyume badala yake yanagusa watu wengi, yanaongelea sehemu pana na unaweza ukakuta mazingira ya kila kaya yapo na ndiyo maana tunasema kubadilisha mtazamo ni muhimu,” anasema Kayombo na kuongeza kuwa:
“Kama mwanzo tulikuwa tunaelewa unyanyapaa uko vipi au changamoto za mila na desturi ziko vipi na tukawa tumesahau mambo ambayo baada ya muda sasa yanajionesha sasa katika jamii zetu ni vizuri sasa tubadili mtazamo na kuona ni namna gani mambo haya yanatoa changamoto katika udhibi wa VVU katika mazingira ya leo na ya hapo baadae.
Jitambue mapema,ingia kwenye huduma maisha yaendelee
Ushauri wa Mwamvita anawasihi wanawake na vijana kutambua hali zao kwa kupima afya ili hata wakikutwa na maambukizi basi waingie kwenye huduma mapema.
“Napenda kuwashuri wanawake wenzangu, vijana na jamii kwa ujumla waende wakapime afya zao mapema ili kama watakutwa na maambukizi basi wajitambue mapema, waingie kwenye huduma maisha yaendelee.
“Nawashauri pia mabinti na wanawake wenzangu kwa ujumla wanapokuwa wanataka kuingia katika mahusiano kwanza wakapime afya zao ndio waingie kwenye mahusiano na iwapo mmoja wao atakataa basi ni vema watumie kondomu.
“Kwani mtu mwenye VVU haonekani wala huwezi kumtambua kwa macho, kwa hiyo tujitahidi kupima na kuwa waaminifu ikiwezekana kuwa na mpenzi mmoja,” anasema Mwamvita.
Mwamvita ni mwanachama wa Taasisi ya Wanawake wanaoishi na Maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI mkoani Kagera inayofahamika kama (AMWAVU).
Kwa sasa AMWAVU wanaendelea na kampeni ya kuhamasisha wanawake kujitokeza kupima saratani ya mlango wa kizazi mkoani Kagera hususan wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Wanawake(UN-WOMEN Tanzania).