8.3 C
New York

Infographic: Elimu zaidi inahitajika chanjo ya corona

Published:

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM  

“Kwa namna hali ilivyo siwezi kuruhusu hata wanangu wachanjwe hii chanjo ya corona, kwani imekuwa na mazingira mengi yanayotia shaka, mfano tumeona kule Uganda Serikali inadanganya ili iweze kupata msaada, hivyo kuwe na mazingira ya uwazi na sisi tutafuata,” anasema Moses George Mkazi wa Kibangu jijini Dar es Salaam.

George anayasema hayo ikiwa ni siku chache tu baada ya chanjo ya corona iliyotolewa kupitia mpango wa COVAX ikiwa tayari imewasili nchini.

Ukweli ni kwamba pamoja na chanjo hiyo ambayo ni dozi zaidi ya milioni moja zilizowasili lakini bado kumekuwa na kusitasita kwa Watanzania linapokuja suala la kuchanjwa kwa ajili ya usalama wao.

Kundi la kwanza ni wale wanaosema kwamba wanaweza kuchanjwa iwapo tu watapata elimu sahihi juu ya chanjo hiyo ikiwamo kuhakikishiwa usalama wao na serikali.

Lakini kundi jingine ni lile linaloamini taarifa za uzushi ambazo zimekuwa zikisambaa mitandaoni kwamba iwapo mtu atapata chanjo ya corona basi madhara yake atayaona baada ya miaka miwili pamoja na kupoteza maisha jambo ambalo siyo kweli.

WANANCHI WANASEMAJE?

Hellen Deogratius ambaye ni mwanafunzi wa elimu ya juu nchini anasema hawezi kukubaliana na chanjo kutokana na mazingira ambayo yamewekwa na serikali hasa kwenye fomu ya mtu anayetakiwa kuchanjwa kwamba haitahusika na madhara yatakayotokea.

“Mimi siwezi kukubaliana na chanjo au kitu chochote ambacho serikali tayari imeweka shaka kwani kama ingekuwa ina imani na hiyo chanjo isingekuwa na haja ya kusema kwamba haitahusika na madhara yatakayotokea baada ya mtu kuchanjwa.

“Mfano ukiangalia chanjo kama ya polio na chanjo nyingine huko nyuma hazikuwa na kipengele kama hicho cha kusema kwamba serikali haitajihusisha na madhara, hivyo hiki ndicho kitu kinachowapa watu wengi wasiwasi na kuamua kulinda usalama wao wenyewe,” anasema Hellen na kuongeza kuwa:

“Kama serikali inashindwa kuchukua jukumu la kuwajibika kutokana na madhara yatakayotokea lazima iwawie watu ugumu wa kuchanjwa, kwani tafsiri yake ni kwamba imejitoa kwenye lawama.

Wakati Hellen akisema hivyo, Moses George ambaye ni mwananchi wa kawaida anasema kuwa bado hayuko tayari kupokea chanjo hiyo kutokana na kuwapo kwa mazingira mengi yanayotia shaka.

“Siyo kwamba hatuhitaji hii chanjo bali kuwapo kwa kipengele kinachosema kwamba serikali haitawajibika na mimi iwapo nitapata madhara hii siwezi kukubalina nayo hata kwa wanangu siwezi kuliruhusu hili litokee labda wachanjwe bila mimi kujua lakini siwezi kuruhusu kuwa sehemu ya majaribio.

“Mfano tumeona kwenye nchi kama Uganda namna ambavyo wanananchi walikuwa wakichanjwa chanjo ambayo si halisia baada ya kulalamika sasa ndio wamesema wataletewa chanjo halisi, kwa mazingira hayo unawezaje kuwa na imani na hiyo chanjo?” anahoji George.

KILICHOTOKEA UGANDA

Juni 30, mwaka huu, washukiwa wawili walikamatwa nchini Uganda kwa kutoa chanjo bandia za Covid19.

Maafisa wanasema kwamba bado haijulikani ni nini kilikuwa kwenye chanjo ambazo walitumia lakini wanafanya uchunguzi juu ya dawa hiyo.

Inaaminika kuwa washukiwa hao wawili huenda waliwachoma chanjo watu takribani 800 katika makampuni binafsi ambayo waliandaa chanjo kwa ajili ya wafanyakazi wake.

Kitengo cha ufuatiliaji kilisema kilipata tetesi kupitia viongozi wa ngazi za chini kuwa wawili hao walizunguka katika maeneo ya Kampala, wakidai ni wafanyakazi wa idara ya afya kutoka hospitali za mwanzo mjini humo.

Hata hivyo, chanjo ya corona nchini Uganda ni bure na zinapatikana katika vituo vya umma na binafsi. Zaidi ya watu 856,000 mpaka sasa wamepatiwa chanjo.

FOMU HIYO INASEMAJE?

Kwa mujibu wa fomu hiyo ya corona iliyotolewa na serikali ilikuwa na kipengele kinachoeleza kuwa ‘Serikali haitawajilibika na chochote kutokana na chanjo hiyo,’.

Maelekezo hayo ni tofauti ukilinganishwa na fomu za nchi nyingine kama Australia ambazo hazina kipengele hicho kilichoonekana kuwashtua Watanzania walio wengi.

SERIKALI YATAKA IAMINIWE

Julai 23, Mwaka huu, Serikali ya Tanzania ilitoa ufafanuzi kuhusu fomu hiyo anayotakiwa kusaini mtu kabla hajapata chanjo.

Fomu hiyo yenye kipengele kinachoeleza kuwa Serikali haitawajibika kwa chochote kutokana na chanjo hiyo.

Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara ya Afya, Dk. Leonard Subi, amesema fomu ni utaratibu wa kawaida katika utoaji wa huduma na kinga kwenye sekta ya afya.

Amesema suala la kusaini fomu ya kuridhia kupata chanjo ni la kawaida na utaratibu huo umekuwa ukifanyika katika mataifa mbalimbali.

“Chanjo si kitu kigeni ndiyo kinga inayoaminika zaidi duniani ndio maana hata Tanzania tumeweza kutokomeza magonjwa kama ndui, pepopunda na mengine.

“Sayansi ya chanjo ni ile ile, hii hofu inasababishwa na watu wanaopinga chanjo na hawa wako duniani kote. Muhimu kuamini Serikali na watalaam na wizara,” amesema Dk. Subi.

VIONGOZI WA DINI

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Fredrick Shoo, akizungumzia chanjo hiyo amesema hatua hiyo ni ya kupongezwa kwa serikali kwani inathamini uhai wa wananchi wake.

“Kwanza niishukuru serikali yetu kwani kwa kufanya hivyo inaonyesha vema kabisa kwamba inajali afya na uhai wa wananchi wake, najua kuna maneno mengi kuhusu chanjo lakini tujue tu kwamba hii siyo chanjo ya kwanza kuwapo duniani hivyo watanzania hawapaswi kuwa na hofu,” amesema Dk. Shoo.

MTAALAM ANENA

Profesa Yunis Mgaya, Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), anasema kuwa kuna faida kubwa kwa mtu anayepata chanjo ya corona ikilinganishwa na yule ambaye hajachanjwa huku akiwataka watanznaia kupuuzia upotoshaji unaoendelea mitandaoni kuhusu chanjo.

“Chanjo ni hatua ambayo inatengenezwa kuwezesha mwili wa binadamu kutopata ugonjwa fulani, na inatengenezwa kufanya mwili utengeneze kinga ili usiugue tena.

“Kuna kinga ambayo unazaliwa nayo na kuna ile ambayo unapata kupitia chanjo, mfano ugonjwa wa ndui, umetokomezwa kwa kutumia chanjo,” anasema Prof. Mgaya.

KUHUSU CHANJO YA CORONA 

Akizungumzia chanjo kwa ujumla, Prof. Mgaya amesema kuwa chanjo haimfanyi mtu asiugue tena lakini inawezesha mwili kuzalisha kinga dhidi ya virusi vya corona.

“Karibu chanjo zote ambazo zimepitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) zina uwezo wa kuzuia usipate ugonjwa mkali wa corona. Kwamba kwa mtu ambaye hajachanja akipata corona inaweza kumpelekea awekwe kwenye mashine na hata kusababisha kifo na hawa ndio wanaojaa hospitali.

“Aliyechanja anaweza kupata maambukizi lakini kiasi cha kinga alichonacho kinazuia makali ya ugonjwa, hivyo hiyo ndio faida kubwa na ndiyo kazi ya chanjo hizi zote zilizopo tofauti na teknolojia na kiwango cha kupambana na virusi,” anasema Prof. Mgaya.

JE NI KWELI AFRIKA INA CHANJO YAKE?

Kuhusu kuwapo kwa ‘minong’ono’ ya Afrika kuwa na chanjo yake tofauti na mabara mengine hususan Ulaya na Marekani na kwamba chanjo hiyo haina ufanisi kama inayoletwa Afrika, Prof. Mgaya anasema kuwa hakuna tofauti badala yake ni mpango wa kutaka kila mmoja apate chanjo hiyo.

“Mpango huu wa COVAX umekuja ukilenga kusaidia nchi ambazo hazina uwezo ili ziweze kupata na ndio maana utaona hata sisi tumepata chanjo ila kusema kwamba ya kwetu ni tofauti hapana, hivyo watanzania waepukane na uvumi huu,” anasema Prof. Mgaya.

MADHARA YA CHANJO

Prof. Mgaya anasema kila chanjo ina aina yake ya madhara na kwamba madhara ni kidogo ikilinganishwa na faida inayopatikana.

“Kila chanjo ina athari kulingana tu na teknolojia iliyotumika kutengeneza na ndio maana hata watu waliokutwa na tatizo la damu kuganda ni wale wenye miaka chini ya 40 na ndio sababu wakasema baadhi ya chanjo zitumike kwa walio na zaidi ya miaka 40.

“Hata matukio ya kuganda kwa damu ni watu wanne (4) kwenye watu 1,000,000 wanaochanjwa ni sawa na kusema kwamba katika kila kundi la watu 250,000 basi ni mtu mmoja ambaye damu itaganda.

“Hata hivyo, kitaalamu athari hizo zinasababishwa na mzio kwamba teknolojia iliyotumika kutengeneza kinga hizo haiendani na miili yao, hivyo athari ni chache kulingana na watu wanavyoongea porojo,” anasema Prof. Mgaya.

MTAZAMO KUHUSU CHANJO

Akizungumzia mtazamo wake kuhusu umuhimu wa chanjo, Prof. Mgaya amesema kuwa hilo siyo jambo la kusubiri kwani lina manufaa kwa umma na kwamba iwapo mtu hayupo tayari kuchoma chanjo basi azingatie kutumia njia zilizoshauriwa na wataalamu wa afya.

“Mimi chanjo ikija hata leo nachanjwa sababu najua faida yake baada ya kuwa nimepata uelewa wa kutosha kwamba chajo hiyo inayengenezwaje na inafaida gani kwenye mwili.

“Hivyo wananchi waondokane na woga wanaojengewa na mitandao ya kijamii, lakini pia chanjo ibakie kuwa hiari ya mtu.

“Muhimu ni mamlaka zenye kuhusika kuendelea kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa chanjo kwa jamii kwa kuelezea faida zake. Pia waeleze ukweli kuhusu uzushi huu uliopo kwenye mitandao ya kijamii kwani umekuwa ukipotosha wengi, kwani kusaidia juhudi za kukabiliana na huu ugonjwa ni kuchanjwa, mamilioni ya watu duniani tayari wameshachanjwa hizo chanjo.

“Kwa mtu ambaye haumwi anatakiwa afahamu kwamba virusi hivi vinabadilika mara kwa mara hivyo hata yule ambaye haumwi hakuna ubaya akiwa na kinga, kuliko kuja kutumia mamilioni mengi ya fedha kwa ajili ya kujikinga,” amesema Prof. Mgaya.

Miongoni mwa waliobahatika kupata chanjo hiyo ni Mbunge wa Nzega Vijijini na aliyewahi kuwa Waziri wa Afya, Dk. Hamis Kingwangalla ambaye anasema kuwa tangu amepata chanjo hiyo hakuna madhara yoyote aliyoyapata.

“Hakuna shida yoyote ambayo nimeipata baada ya chanjo, lakini niseme tu kwamba chanjo hii ni hiari hakuna anayelazimishwa, ukiona utapona kwa kujifukiza sawa au kwa njia yoyote ile unayoona kwako ni sahihi sawa,” amesema Dk. Kigwangalla.

CHANJO YA HAINA MADHARA

Akizungumzia kuhusu kuwapo kwa ripoti inayosambaa kuwa asilimia 60 ya waliolazwa kwa Covid-19 nchini Uingereza walishapata chanjo zote, Prof. Mgaya amesema kuwa hizo ni sehemu ya porojo zinazoendelea.

“Hizo ni porojo tu, hakuna kitu kama hicho kwani kama tutashindwa kudhibiti taarifa hizi za uzushi zitatupa changamoto, hivyo Watanzania waachane nazo,” amesema Prof. Mgaya.

Kuhusu chanjo ya Johnson and Johnson iliyoletwa nchini ambayo inaelezwa kuwa ilishasitishwa kwenye baadhi ya Mataifa baada ya kuonekana ina madhara ambapo amesema kuwa chanjo hiyo iko salama.

“Hizo ni porojo tu kwani chanjo hiyo ilistishwa kwa siku 7 tu wakati wakijiridhisha, Wamarekani milioni 13 wameshachanjwa na hiyo, hata ukitembelea kwenye tovuti yao ya Jahson utaona, hivyo Tanzania haiwezi kuleta chanjo ambayo imepigwa marufuku, hakuna. Juzi tu hapa New Zealand ameishukuru kw akupata chanjo hii, hivyo Watanzania waache kupotoshwa.

HALI HALISI

Kwa mujibu wa taarifa ya mwisho iliyotolewa na serikali kupitia Wizara ya Afya, hadi sasa Tanzania inawagonjwa 858 wa corona huku vifo vikiwa ni 29.

Hivyo ni muhumu kwa kila mmoja kuchukua tahadhari zote muhimu ili kujinusuru na ugonjwa huu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img