12.9 C
New York

Nani kumrithi Guterres kiti cha Katibu Mkuu UN?

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, atamaliza muda wake Desemba, 2026, na tayari mbio za kusaka mrithi wake zimeshaanza.

Guterres amekuwa katika nafasi hiyo ya Katibu Mkuu tangu mwaka 2017 na sasa baadhi ya wanadiplomasia na wanasiasa wakubwa duniani wanawania nafasi ya kuvaa viatu vyake.

Ifahamike kuwa Katibu Mkuu mpya wa UN ataanza majukumu yake Januari Mosi, 2027, ambapo ataongoza kwa miaka mitano, kisha muhula wa pili (wa miaka mitano) endapo atavuna ushawishi hapo baadaye.

Je, ni nani anayepewa nafasi kubwa ya kuchaguliwa na Mkutano Mkuu? Makala haya yanachambua wanadiplomasia na wanasiasa maarufu wanaowania nafasi hiyo nyeti ndani ya UN.

RAFAEL GROSSI

Mwanadiplomasia wa Argentina mwenye umri wa miaka 65, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomic duniani (IAEA).

Ushawishi wake unatokana na ushiriki wake mkubwa katika masuala ya kimataifa, ikiwamo mgogoro wa nyuklia kati ya Iran na Marekani.

Pia, Grossi ameshiriki katika vita vya Urusi na majirani zao, Ukraine, kwa kutuma timu yake kwenye eneo la Zaporizhzhia lenye kituo cha uzalishaji wa nyuklia.

REBECA GRYNSPAN

Umri wake ni miaka 70. Ni Makamu wa Rais wa zamani wa Costa Rica na sasa ni Mkuu wa Mkutano wa Biashara na Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNCTAD).

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa, Grynspan ameachana na kiti hicho ndani ya UNCTAD ili kuepusha mgongano wa masilahi katika nafasi ya Katibu Mkuu wa UN anayoitaka.

Endapo atachaguliwa, Grynspan, ambaye ni muumini wa mahusiano ya kimataifa, amani na haki za binadamu, atakuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya Katibu Mkuu wa UN.

MICHELLE BACHELET

Rais wa zamani wa Chile na aliwahi kuwa Kamishina wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, pia akiongoza Baraza la Wanawake la UN kuanzia mwaka 2010 hadi 2013.

Kampeni zake za kuwania nafasi ya Katibu wa UN ilikuwa kizingiti baada ya Taifa lake la Chile kutangaza kuwa haliko upande wake.

Hata hivyo, anaungwa mkono na Brazil na Mexico, licha ya baadhi ya wanasiasa wa Marekani kulaani kitendo chake cha kutetea haki ya utoaji mimba.

MACKY SALL

Umri wake ni miaka 64. Alikuwa Rais wa Senegal kwa miaka 12, kabla ya kuondoka madarakani mwaka 2024.

Akiiongoza Senegal, Sall aliiwezesha nchi hiyo kutekeleza miradi mingi ya ujenzi wa miundombinu, pia akizipa ushirikiano mkubwa nchi zenye changamoto ya madeni.

Katika kampeni zake kuwania kiti cha Katibu wa UN, amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kushirikishwa ndani ya Umoja huo. Endapo atachaguliwa, atakuwa Mwafrika wa tatu kushika nafasi hiyo.

MARIA FERNANDA ESPINOSA

Ni Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Ecuador, pia akiwahi kushika nafasi ya Waziri wa Ulinzi wa Taifa hilo la Amerika ya Kusini.

Espinosa, ambaye ni mgombea mdogo zaidi kwa umri wake wa miaka 61, amewahi kuwa Balozi wa Ecuador ndani ya UN na Rais wa Mkutano Mkuu wa Umoja huo.

Amekuwa akisisitiza umuhimu wa UN kushughulikia migogoro kabla haijaanza. Pia, anafahamika kuwa ni mwanaharakati nguli wa mabadiliko ya hali ya hewa.

Related articles

Recent articles